1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump auponda uteuzi wa Harris mgombea kama mwenza wa Biden

12 Agosti 2020

Muda mchache baada ya mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic, Joe Biden, kumtangaza Seneta Kamala Harris, kuwa mgombea mwenza wake, Rais Donald Trump ameukosoa uteuzi huo kuwa umekwenda kombo.

https://p.dw.com/p/3gq3q
US-POLITICS-CUSTOMS AND BORDER-HEARING
Picha: Getty Images/AFP/A. Drago

Biden alimtaja Kamala Harris kama mwanamke asiyeogopa na mtumishi wa umma aliyetukuka. "Ni fakhari kwangu kuwa na mshirika huyu kwenye kampeni zetu," alisema Biden mwenye umri wa miaka 77 wakati akitangaza jina la seneta huyo wa Carlifornia. 

Uamuzi huu uliotangazwa kupitia njia mashuhuri ya mwaka huu wa 2020, yaani mitandao ya kijamii, umekuja kwenye kipindi muhimu kwa Biden anayetaka kujenga muungano wa makundi mbalimbali ili kumshinda Trump, chini ya miezi minne kabla ya uchaguzi wenyewe.

Kamala Harris, mwenye umri wa miaka 55, anaweza kuwavutia zaidi wanawake na vijana hasa kutokea kwenye viunga vya mijini, ambao uchunguzi wa maoni unaonesha kwamba wamekuwa wakimkimbia Trump.

Hata hivyo, Trump mwenyewe ameukosowa vikali uteuzi huo, akimtaja mwanasheria huyo aliyegeuka kuwa mwanasiasa kama mtu mwoga na asiyefaa.

"Alikuwa mmoja wa watu waliotabiriwa kuwa na nafasi ya kushinda. Lakini alichofanya ni kuwa baada ya watu kumjuwa, akaporomoka. Alimazia na asilimia 2, na yumkini chini ya hapo. Kisha akakimbia. Kumbuka jinsi alivyokuwa na pupa ya kusema maneno mabaya dhidi ya Biden. Kitu pekee ambacho sifikirii kama yeye Biden angeliweza kukifanya. Yaani anamchukuwa mtu ambaye alimuita mbaguzi," alisema Trump.

Tuhuma za Trump si sahihi

Ukweli ni kwamba Kamala Harris hakuwahi kutowa kauli hiyo wakati alipokuwa kwenye mdahalo wa kuwania uteuzi wa kugombea urais kwa chama cha Democrat, na badala yake alisema: "Siamini kama wewe ni mbaguzi" kabla hajamkosowa kwa jinsi Biden alivyokuwa akipinga sera zinazoondosha mfumo wa ubaguzi kwenye skuli.

USA Kamala Harris  Primaries Debatte mit Biden
Kamala Harris (kulia) akiwa kwenye mdahalo na Joe Biden mwezi Julai 2019, wote wakiwania uteuzi wa kugombea urais kwa tiketi ya Democrat. Picha: picture-alliance/AP Photo/P. Sancya

Debbie Walsh, mkurugenzi wa Kituo cha Wanawake wa Kimarekani na Siasa cha Chuo Kikuu cha Rutgers, amemuelezea Kamala Harris kama chaguo bora kabisa kwa makamu wa rais wa Marekani.

"Kwa hakika, ni chaguo la kihistoria. Anakuwa mwanamke wa nne kuwania nafsi kubwa kama hiyo kisiasa, lakini wa kwanza asiyekuwa mzungu. Wa kwanza mwenye mchanganyiko wa rangi, wa kwanza wa Kiafrika na wa kwanza wa Asia Kusini. Kinachosisimua kwenye uteuzi huu ni kwamba unabadilisha mustakabali wa muonekano wa chama cha Democrat."

Kamala Harris, ambaye mama yake aliingia Marekani kusomea shahada ya uzamifu kwenye masuala ya sayansi akitokea Tamil Nadu nchini India na baba yake na Mjamaika mwenye asili ya Afrika, amemshukuru Biden kwa uteuzi huo akisema ni jambo la heshima kubwa kwake na kwamba atafanya kila awezalo kumsaidia. 

"Joe Biden anaweza kuwaunganisha Wamarekani kwa sababu ametumia maisha yake kutupigania. Na akiwa rais, ataijenga Marekani inayoakisi matazamio yetu," aliandika kwenye mtandao wa Twitter.