1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Trump ashtakiwa kwa kujaribu kutengua uchaguzi wa 2020

2 Agosti 2023

Donald Trump amefunguliwa mashtaka kuhusiana na juhudi zake za kuyabatilisha matokeo ya uchaguzi wa Marekani wa 2020. Ni kitisho kikubwa kabisa cha kisheria kwa rais huyo wa zamani anayetaka kurejea Ikulu ya White House

https://p.dw.com/p/4UfCk
USA Wahlen 2024 Donald Trump
Trump anakabiliwa na mashitaka kadhaa mahakamani wakati kampeni za uchaguzi wa 2024 zikishika kasiPicha: Sue Ogrocki/AP Photo/picture alliance

Ni shtaka la tatu la jinai kwa Trump mwenye umri wa miaka 77 tangu mwezi Machi mwaka huu na mara hii anashtakiwa kwa makosa matatu ya kula njama na moja la kuzuia mkondo wa sheria.

Soma pia: Majaji kumchunguza Trump kwa jaribio la kupindua uchaguzi

Trump, mgombea anayeongoza katika kinyang'anyiro cha uteuzi wa tiketi ya urais ya chama cha Republican kwa uchaguzi wa 2024, tayari amepangiwa kufikishwa mahakamani jimboni Florida Mei mwaka ujao kwa madai ya kuzitumia vibaya nyaraka za siri za serikali.

Mashtaka hayo mapya, ambapo mawili kati ya hayo yana hukumu za vifungo vya juu vya miaka 20 jela, yanaongeza uwezekano wa Trump kujikuta katika kesi Zaidi za kisheria katika kilele cha kile kinachotarajiwa kuwa kampeni kali ya urais.

USA Staatsanwalt Jack Smith
Mwanasheria Jack Smith alisoma shtaka dhidi ya TrumpPicha: Jacquelyn Martin/AP Photo/picture alliance

Shtaka hilo lililotangazwa na mwanasheria maalum Jack Smith linamtuhumu Trump kwa njama ya kuilaghai Marekani na njama ya kuzia mchakato rasmi – ambao ni kikao cha Pamoja cha bunge la Congress cha Januari 6, 2021 kilichoandaliwa kuidhinisha ushindi wa Joe Biden. Smith, mwendesha mashitaka wa zamani wa uhalifu wa kivita mjini The Hague, amesema shambulizi la Januari 6 la wafuasi wa Trump katika jengo la Bunge la Capitol ilikuwa shambulizi ambalo halijawahi kushuhudiwa kwenye makao makuu ya demokrasia ya Marekani. "Wanaume na Wanawake wa vikosi vya usalama waliolilinda jengo la bunge la Marekani mnamo Januari 6 ni mashujaa. Ni wazalendo na ni bora zaidi katika jamii. Hawakulinda tu jengo au watu waliojificha humo. Waliyaweka maisha yao hatarini ili kuilinda nchi pamoja na watu wake."

Soma pia: 

Trump pia anatuhumiwa katika shtaka hilo lenye kurasa 45 kwa kutaka kuwanyima wapiga kura wa Marekani haki yao ya uchaguzi wa haki kwa kueneza madai ya uwongo kuwa alishinda uchaguzi wa rais wa Novemba 2020  

Ikulu ya White House imesalia kimya kuhusiana na shtaka hilo la kihistoria dhidi ya Trump. Biden, anayefanya kampeni za kutaka kuchaguliwa tena mwaka ujao, aliendelea na likizo yake ya ufukweni jimboni Delaware, na mkewe Jill Biden.

USA Jacob Anthony Chansley Gewaltsamer Einbruch Capitol Verschwörungstheoretiker
Wafuasi wa Trump walivamia Capitol Hill Januari 6, 2021Picha: Douglas Christian/Zumapress/picture alliance

Timu ya kampeni ya Trump, wakati huo huo, ilitoa taarifa kali, ikiilinganisha mashtaka yake na iliyokuwa Ujerumani ya Kinazi katika miaka ya 1930, na kusema kuwa alifuata ushauri kutoka kwa wanasheria wenye tajriba kubwa.

Shitaka hilo linawataja washiriki sita lakini hakuna aliyetambulishwa kwa jina na Trump, ambaye anatarajiwa kufikishwa kizimbani kesho Alhamisi, ndiye mshitakiwa pekee aliyetambulishwa.

Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa na Jaji wa Mahakama ya Wilaya nchini Marekani Tanya Chutkan, aliyeteuliwa na rais wa zamani Mdemocrat Barack Obama. Smith amesema anataka kesi hiyo ifanywe haraka.

Trump amemsuta mwanasheria huyo maalum, akimuita kuwa aliyechanganyikiwa na kumtuhumu kwa kile alichokiita shtaka jingine bandia ili kuingilia uchaguzi wa rais.

Ameandika kwenye mtandao wake wa Truth Social kuwa kwa nini hawakuyafanya hayo miaka miwili na nusu iliyopita? Kwa nini walisubiri muda mrefu?

Pence ambaye anashindana na Trump katika mchujo wa chama cha Republican, amesema kwenye mtandao wa X, ambao awali ulifahamika kama Twitter, kwamba shitaka hilo linatumika kama ukumbusho muhimu: mtu yeyote anayejiweka juu ya Katiba hafai kamwe kuwa Rais wa Marekani.

afp, reuters