1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aongeza ushuru kwa bidhaa za China

Yusra Buwayhid
11 Mei 2019

Rais wa Marekani ametangaza kuziwekea ushuru wa mabilioni ya dola bidhaa zilizosalia za China. Hatua hiyo imekuja kati kati ya mazungumzo baina ya nchi hizo mbili, ya kujaribu kuutuliza mgogoro wao wa kibiashara.

https://p.dw.com/p/3IL78
USA Wirtschaft l Handelsbilanz
Picha: Getty Images/AFP/M. Ralstone

Rais Donald Trump wa Marekani, ameagiza kuongezwa kwa ushuru kwa karibu bidhaa zote za China zilizosalia na zinazokadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 300.

Uamuzi wa Trump unakinzana na kauli zake alizoziandika katika ukurasa wa Tweeter. Trump aliandika awali kwamba mazungumzo ya siku mbili za nyuma yalikuwa na uwazi pamoja na mafanikio.

"Uhusiano baina yangu na Rais Xi (Jinping) bado ni mzuri sana, na mazungumzo kuhusu mipango ya siku za mbele itaendelea," ameendelea kuandika Trump katika ukurasa wa Tweeter.

"Ushuru dhidi ya China huenda ukaondolewa au usiondolewe, itategemea namna mazungumzo ya siku za mbele yatakavyokuwa!

Mwakilishi wa mazungumzo hayo ya kibiashara kwa upande wa China, makamu wa waziri mkuu Liu He kwa upande wake amewaambia waandishi habari kwamba mazungumzo yalikuwa mazuri, na kwamba pande mbili zitakutana tena mjini Beijing, China bila ya kutaja tarehe maalumu, lakini pia alionya kwamba China haitokubali madai ya Marekani katika vipengele muhimu vya mazungumzo hayo.

"Mazungumzo hayajavunjika," alisema Liu.

Matamshi ya aina hiyo - yaliyotolewa kabla ya Trump kuamrisha duru nyingine ya kuiongezea China ushuru- yalitoa matumaini hasa katika katika Soko la Hisa la Wall Street mjini New York, Marekani. Hisa zilipanda baada ya biashara kuwa katika hali ya wasiwasi wiki nzima.

Matumaini yasambaratika

Matumaini hayakudumu kwa muda mrefu, mfanyabiashara huyo aliyegeuka kuwa rais wa Marekani, alibadilisha mawazo na kutekeleza vitisho vyake ambavyo amekuwa akivitoa kwa miezi kadhaa.

Uamuzi huo wa Trump alioutoa kupitia kupitia ukurasa wake wa Tweeter hapo Ijumaa, umezidi kongeza mvutano wa kibiashara baina ya Marekani na China inayoshikilia nafasi ya pili kwa kuwa na uchumi mkubwa duniani.

"Rais ametuamrisha kuanza mchakato wa kuziongezea ushuru takriban bidhaa zote zilizosalia za China, ambazo zinakadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 300," amesema mwakilishi wa Biashara Marekani Robert Lighthizer katika tamko rasmi.

Kauli ya Trump, pia imetolewa takriban siku moja tangu Marekani iamue kuongeza ushuru kwa bidhaa za Kichina zenye thamani ya dola bilioni 200, ikiwa ni ongezeko la asilimia 25 kutoka asilimia 10 ya hapo awali.

Adhabu hiyo imetolewa baada ya Rais Trump kuituhumu China kukwepa majukumu yake. Kutokana na hatua hiyo, China imesema mazungumzo yataendelea ili kutafuta suluhisho la mgogoro huo. Awali Liu alionya awali kwamba China lazima iitikie uamuzi wowote wa Marekani wa kuingezea ushuru bidhaa zake.

Maelezo zaidi kwa umma kuhusu mpango huo wa kuziongezea ushuru bidhaa zaidi za China yatatolewa Jumatatu, kabla ya kutolewa uamuzi wa mwisho, amesema Lighthizer.

Trade Talks zwischen USA und China
makamu wa waziri mkuu Liu He (Kati kati) akizungumza na Waziri wa Fedha wa Marekani Steven Mnuchin (Kulia) na Mwakilishi wa Biashara Robert Lighthizer (Kushoto)Picha: Reuters/N. Asfouri

Marekani imefanya uamuzi wake huo baada ya kumalizika siku mbili za mazungumzo ambayo yalishindwa kufikia maafikiano, lakini pia bila mazungumzo hayo hayakuwa yamevunjika. Kulikuwa bado kuna matumaini kuwa Marekani na China zingeweza kufikia maafikiano ya aina fulani na kueousha kuuweka hataraini uchumi wa dunia.

Waziri wa Fedha Steven Mnuchin na Lighthizer walikutana kwa masaa mawili Ijumaa, na baadae kuelekea Ikulu ya Marekani kumtaarifu Trump kuhusu mkutano wao huo, ambaye alisema hana haraka ya kufikia makubaliano, na kudai kwamba Marekani inafanya majadiliano ikiwa katika nafasi nzuri ya kufanikiwa.

Vipengele vilivyokosa mafikiano

Liu naye alisema kwamba wamekubaliana vipengele kadhaa, lakini pia kuna vipengele walivyoshindwa kukubaliana ambavyo wanaamini vinahusu masuala muhimu sana.

Liu ameainisha mambo muhimu walioshindwa kukubaliana ni: iwapo ushuru uliootangazwa wakati wa mgogoro utafutwa watakapofikia makubaliano, kiwango hasa cha manunuzi ya China cha bidhaa za Marekani, na maandishi ya makubaliano yenye usawa.

Yang Delong mwanauchumi huko Shanghai, China ameliambia shirika la habari la AFP kwamba sababu iliyomfanya Trump ghafla kubadili kauli ni uchaguzi wa rais wa Marekani wa 2020.

Mwaka uliopita, Marekani na China ziliongezeana ushuru uliopindukia dola bilioni 360 katika biashara zao, na kuuathiri uchumi wa nchi zote mbili.

Liu amelinganisha mazungumzo yao na mbio za marathon: "Unapofikia karibu na mwisho hali inazidi kuwa ngumu, ni wakati wa giza kabla ya mapambazuko."