1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump amfuta kazi Mwanasheria Mkuu

31 Januari 2017

Rais wa Marekani Donald Trump amemfukuza kazi Kaimu Mwanasheria Mkuu nchini humo Sally Yates ambaye aliwaagiza watumishi wa idara hiyo kutofanyia kazi agizo la kuzuia wasafiri wanaotokea mataifa saba ya Kiisilamu

https://p.dw.com/p/2Wh3M
Washington Sally Q. Yates Vize-Justizministerin
Sally Yates, Kaimu Mwanasheria Mkuu wa Marekani aliyefukuzwa na Rais TrumpPicha: Getty Images/P. Marovich

 

Katika taarifa yake Ikulu ya Marekani, White House imesema mwanasheria mkuu Sally Yates ni dhaifu katika kushughulika masuala ya mpakani na suala linalohusiana na wahamiaji haramu nchini humo huku pia ikikikosoa chama cha Democratic kwa kushindwa kuidhinisha kwa wakati uteuzi wa Jeff Sessions aliyetarajiwa kushika wadhifa huo wa mwanasheria wa serikali.

Tayari nafasi ya mwanasheria huyo imejazwa ambapo Dana Boente ameteuliwa kukaimu nafasi. Isaac Gamba anarifu zaidi katika taarifa ifuatayo

Katika taarifa hiyo Ikulu ya White House imesema Bibi Yates amekwenda kinyume na wajibu wa idara yake baada ya kukataa kuidhinisha agizo la kisheria maalumu kwa ajili ya kulinda usalama wa raia wa Marekani.

Kutokana na hatua hiyo Mwendesha Mashitaka Dana Boente atakaimu nafasi hiyo hadi pale seneta Jeff Session  atakapokuwa amethibitishwa na seneti.

Yates alitilia shaka uhalali wa amri ya Trump

Katika waraka wake kwa watumishi wa idara hiyo, Yates ambaye ni mwanasheria wa serikali aliyeteuliwa na aliyekuwa rais wa nchi hiyo Barack Obama alielezea mashaka yake kuhusiana na uhalali wa kisheria juu ya agizo hilo la Trump ambalo limekumbana na upinzani mkali.

Karikatur von Sergey Elkin zu Trump Einreiseverbot (türkisch)
Maoni ya mchoraji wa vibonzo kuhusu hatua anazozichukua Rais Trump

Alisema akiwa ni kaimu mwanasheria mkuu wa serikali hawezi kutekeleza maagizo ambayo ana mashaka nayo hadi pale atakapokuwa amejiridhisha kuwa hayaendi kinyume na misingi ya kisheria.

Maelekezo yaliyotolewa na Yates yaliashiria kuwa serikali ya Trump isingekuwa na uwakilishi wa kisheria katika mashauri ambayo yanalenga kupinga agizo hilo la Rais Donald Trump.

Saa chache baada ya kuteuliwa kukaimu nafasi hiyo ya mwanasheria mkuu wa serikali, Dana Boente alisema atatetea uamuzi huo wa Rais Trump.

Wamarekani wa asili ya Iran wajawa na wasiwasi

Wakati huo huo jamii ya Wamarekani wenye asili ya Iran wanaoishi katika jimbo la California wameelezea wasiwasi wao kuhusiana na agizo hilo la Trump la kuwazuia wahamiaji wanaotoka mataifa saba yenye idadi kubwa ya Waislamu kuwa litazisambaratisha familia za jamii ya watu wa mataifa hayo na kuchafua taswira ya Marekani kimataifa.

Kiasi ya watu 300,000 hadi 500,000 wenye asili ya Iran wanaishi kusini mwa California na kuna uwezekanano mkubwa wakaguswa kwa njia moja ama nyingine na agizo hilo.

Wakati huo huo, aliyekuwa Rais wa Marekani, Barack Obama amekosoa vikali  hatua ya Rais Trump kuhusiana na kupiga marufuku wahamiaji na wasafiri kuingia nchini humo.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE

Mhariri: Grace Patrciia Kabogo