1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump alihutubia taifa

6 Februari 2019

Rais Donald Trump wa Marekani amesema kwenye hotuba ya hali ya taifa kwamba mkutano wa pili wa kilele kati yake na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un utafanyika Februari 27 na 28 nchini Vietnam.

https://p.dw.com/p/3Cn9K
USA Ansprache zur Lage der Union in Washington
Picha: Reuters/J. Young

Rais Donald Trump wa Marekani amesema mkutano wa pili wa kilele kati yake na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un utafanyika Februari 27 na 28 nchini Vietnam. Rais Trump amesema wakati wa hotuba yake ya hali ya taifa mapema Jumanne.

"Tunaendelea na shinikizo letu la kihistoria la amani katika rasi ya Korea "aliliambia Baraza la Congress katika hotuba yake hiyo iliyoangazia hali ya kitaifa, na kuongeza kuwa "mateka wetu wamerudi, majaribio ya nyuklia yamesitishwa na hakujakuwepo na kombora lililorushwa kwa miezi 15. Kama nisingechaguliwa rais wa Marekani kwa maoni yangu nadhani tungekuwa tumeingia kwenye vita kubwa na Korea Kaskazini", alisema Trump.

Wakuu hao walikutana kwa mara kwanza katika mkutano wa kilele mwezi Juni nchini Singapore, ikiwa ni mara ya kwanza kwa rais wa Marekani kukaa pamoja na kiongozi wa Korea Kaskazini.

Donald Trump und Kim Jong Un Singapur
Donald Trump na Kim Jong Un walipokutana nchini SingaporePicha: Reuters/K. Lim

Aidha rais Trump ametumia hotuba hiyo kuliomba bunge kumaliza mkwamo wa muda mrefu wa kisiasa. Trump amesema pamoja na mafanikio ya kila wakati ya taifa hilo, lakini bado lina wajibu wa kutengeneza mfumo wa wahamiaji utakaolinda maisha na kazi za raia wa Marekani.

Amesisitiza kuhusu umoja miongoni mwa watu wa Marekani, akitaka mabadiliko baada ya miaka miwili ya mivutano. "Ajenda nitakayoileta leo sio ya WaRepublican ama WaDemocrat. Ni ajenda ya watu wa Marekani," ameongeza Trump.

Trump kama iliyotarajiwa alitoa hotuba hiyo kwa sauti iliyoonyesha umoja, licha ya mvutano wa hivi karibuni na Wademocrats juu ya suala la fedha za ujenzi wa ukuta wa mpaka na Mexico, na kusababisha kufungwa kwa shughuli za serikali kwa muda mrefu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya taifa hilo.

Während einer Begrüßungszeremonie in der Großen Halle des Volkes in Peking wird neben dem chinesischen Emblem eine amerikanische Flagge gezeigt
Marekani na China wamekuwa katika hatua kadhaa za kumaliza mzozo mkubwa wa kibiashara kati yaoPicha: picture-alliance/A. Wong

Kwenye hotuba yake hiyo, amegusia pia mafanikio makubwa ya kiuchumi na kusema amekuwa katika mstari ulio sawa kwa kuanzisha sera mpya na ngumu za biashara zilizoziingiza Marekani na China kwenye vita vya kibiashara, huku akiwataka WaRepublican na Democrats kushirikiana ili kuujenga uchumi wa Marekani uliotetereka.

Aidha, rais Trump amezungumzia juhudi zake za kukubaliana upya mikataba ya kibiashara na China na mataifa mengine, kwa lengo la kuyafanya makubaliano hayo kuiependelea zaidi Marekani. Amesema, ili kufanikiwa kuujenga uchumi mkubwa wa taifa hilo, suala kubwa na muhimu zaidi ni kuzibadilisha sera mbovu za biashara.

Kuhusu mazungumzo na makundi ya Afghanistan, rais Trump amesema serikali yake inaendeleza mazungumzo ya kujenga na makundi hayo, ikiwa ni pamoja na Taliban, na kuna uwezekano wa  kupunguza wanajeshi wake nchini humo na kujikita kwenye mapambano dhidi ya ugaidi unaozidi kushika kasi.

Hata hivyo amesema ana wasiwasi kuhusu iwapo watafikia makubaliano, lakini wanaamini kwamba baada ya miongo miwili ya vita, umefika wakati wa kujaribu kusaka suluhu ya amani, alisema Trump kwenye hotuba hiyo.

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/AFPE

Mhariri: Caro Robi