1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump akutana na Mwanamfalme bin Salman

21 Machi 2018

Rais wa Marekani Donald Trump amemkaribisha kwa heshima zote kiongozi mwenye mamlaka makubwa wa Saudi Arabia, mwana Mfalme Mohammed bin Salman

https://p.dw.com/p/2ugVU
USA Mohammed bin Salman, Kronprinz Saudi-Arabien & Donald Trump in Washington
Mwana mfalme Mohammed bin Salman akiwa na Rais Donald TrumpPicha: Reuters/JE. Vucci

Rais wa Marekani Donald Trump kasifu mauzo ya zana za kivita za Marekani kwa Saudia kuwa zinapanua wigo wa ajira za raia wa taifa lake, pamoja na taifa hilo kukosolewa vikali katika ushiriki wake katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen. 

Katika hafla hiyo Trump na mwana mfalme wamesifu uthabiti wa ushirikiano wa mataifa yao, ambao ulikuwa umedhoofika katika utawala wa Obama, na hasa kutokana na kutofautiano katika masuala kadhaa likiwemo la kikanda la taifa hasimu na Saudi Arabia la Iran katika kanda hiyo.

Sio Trump pekee, ambaye amechukuwa msimamo mkali dhidi ya Iran lakini pia mwana mfalme wa Saudia, yeye akimlinganisha Kiongozi mkuu wa Iran na  Adolf Hitler. Wachambuzi wanasema hatua ya Trump kumwekea zulia jekundu ni ishara kuwa serikali yake inamuunga mkono kiongozi huyo ambaye aliendesha kampeni kubwa dhidi ya rushwa iliyoimarisha utawala wake na sera zake za kigeni kuondosha tofauti na washirika miongoni mwa mataifa ya Magharibi. Wakati huo huo taifa hilo la kifalme kuonekana kama limekumbwa na upepo mpya wa mabadiliko ya uhuru wa kijamii kutokana na kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 32, baada ya miongo kadhaa ya viongozi waliopita.

Mipango ya biashara ya silaha

USA Mohammed bin Salman, Kronprinz Saudi-Arabien & Donald Trump in Washington
Mkutano wa bin Salman na Rais TrumpPicha: Getty Images/AFP/S. Loeb

Mwaka uliopita Rais Trump na mwana Mfalme Mohammed walijadili makubaliano ya uwekezaji wa Saudi Arabia wa thamani ya dola bilioni 200 nchini Marekani, yakiwemno ya ununuzi wa zana za kijeshi. Trump amesema manunuzi hayo yamechangia uundwaji wa ajira mpya 40,000 nchini mwake. Kiongozi huyo wa Marekani alionesha vielelezo vya manunuzi ya vifaa hivyo vya kijeshi vya Saudi Arabia, kuanzia meli, makombora, ndege hadi magari.

Naye mwana Mfalme Mohammed bin Salman alisema"Nina imani hii fursa ni kubwa sana. Na tunaendelea kushughulikia fursa nyingine mpya na tunaendelea kuandaa ziara ya Mfalme haraka iwezekanavyo kutokana na wimbi jipya la fursa katika maeneo mengi. Na tunaamini tunaweza kufanya mengi makubwa kwa pamoja."

Baadaye akizungumza na waandishi wa habari rais Trump alisikika akisifu " Saudi Arabia ni taifa tajiri sana, na linatarajia kuipa Marekani kiasi cha utajiri wake, natumani ni katika namna ya ajira, katika namna ya manunuzi ya vifaa bora vya kijeshi duniani."

Mwana Mfalme Mohammed bin Salman ambae pia ni waziri wa ulinzi katika ziara yake hiyo ya kusaka uwekezaji ya Marekani itamfikisha New York, Boston, Seattle, Los Angeles, San Francisco na Houston.

Wakati ziara hiyo ikiendelea maseneta nchini Marekani wapo katika mjadala wa kutafutia ufumbuzi wa kuitaka Marekani kutoiunga mkono kampeni ya Saudi Arabia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Yemen ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 10,000. Baadhi ya wabunge wa bunge la Marekani wameonesha ukosoaji mkali kwa namna Saudia inavyoshiriki katika vita hivyo na hasa kutokana na hali ya kiutu na vifo vya raia.

Mwandishi: Sudi Mnette/RTR
Mhariri:Josephat Charo