Trump akubali Urusi ilifanya udukuzi
8 Januari 2017Rais Mteule wa marekani Donald Trump ameikubali ripoti ya ujasusi kwamba Urusi ilihusika katika mashambulizi ya mitandao yaliyolenga kuvuruga uchaguzi wa Marekani.
Mkuu mtarajiwa wa shughuli za ikulu katika serikali ya Trump Reince Priebus amesema na kuongeza huenda hatua zikachukuliwa.
Akizungumza na shirika la habari la FOX siku ya Jumapili, Priebus amesema Trump anakubali kuwa kuhusu hoja hii, ni taasisi za Urusi ambazo zilihusika na uingiliaji huo wa mpangilio na shughuli katika chama cha Democratic.
Priebus amesema Trump anapanga kuziagiza taasisi za ujasusi kutoa mapendekezo ya kuhusu kile kinachostahili kufanywa. Kwa kutegemea mapendekezo hayo, hatua zinaweza kuchukuliwa.
Lakini timu ya mpito ya Donald Trump imekilaumu chama cha Democratic kwa kuruhusu anwani za barua pepe zao zao kudukuliwa. Timu hiyo imepuuzilia mbali ripoti za mashirika ya ujasusi kwamba Urusi iliingilia mchakato wa uchaguzi.
Naye Rais Barrack Obama amekiri kuwa hakutiilia uzito athari ambazo habari potofu za udukuzi zinaweza kuhujumu demokrasia ya nchi, kauli inayojiri baada ya ripoti ya ujasusi kuhusu hatua ya Urusi kuingilia kati uchaguzi wa Marekani.
Akihojiwa na shirika la habari la ABC, Obama amemtahadharisha mrithi wake anayechukua hatamu za uongozi katika muda wa wiki mbili zijazo Donald Trump kuhusu tofauti kati ya kampeni na utawala, huku akisema rais mteule hataendesha urais kama anavyoendesha biashara ya kinyumbani.
Mahojiano hayo ya Obama yalirekodiwa Ijumaa. Siku ambayo pia shirika la ujasusi lilitoa ripoti mpya iliyosema kuwa Rais wa Urusi Vladimir Putin aliagiza kampeni ya udukuzi kufanywa na kuzifichua taarifa za siri na porojo kupitia vyombo vya habari kwa lengo la kumhujumu aliyekuwa mgombea wa urais wa chama cha Democratic Hillary Clinton.
Mwandishi: John Juma/RTRE/AFPE/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga