1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump asema Saudi Arabia isihukumiwe

17 Oktoba 2018

Rais wa Marekani Donald Trump ameitetea Saudi Arabia kuhusiana na kupotea kwa mwandishi habari Jamal Khashoggi. Trump ameonya kwamba hakuna haja ya kuihukumu nchi hiyo

https://p.dw.com/p/36fOO
USA | Trump über das Abkommen USMCA zwischen USA und Kanada
Picha: Reuters/K. Lamarque

Rais huyo wa Marekani badala yake amesema ni vyema kila mmoja akawa na subira hadi uchunguzi kuhusiana na suala hilo utakapokamilika.

Kwenye mahojiano na shirika la habari la Associated Press, Trump amekifananisha kisa cha Khashoggi ambaye maafisa wa Uturuki wanasema aliuwawa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul, na madai ya udhalilishaji wa kingono dhidi ya hakimu wa mahakama ya juu wa Marekani Brett Kavanaugh.

Trump amesema na hapa nayanukuu maneno yake, "nafikiri tunastahili kujua kilichotokea kwanza. Hapa tena, ni kile kisa cha mtu kuwa na hatia mpaka atakapothibitishwa kwamba ni msafi. Tumeshuhudia kitu kama hiki na hakimu Kavanaugh na hana hatia siku zote kulingana na mimi," mwisho wa kunukuu.

Gazeti la Uturuki limechapisha taarifa ya jinsi Khashoggi alivyouwawa

Kauli hii ya Trump ndiyo ya wazi kabisa ambapo anaonesha kuitetea Saudi Arabia, nchi ambayo ameifanya kuwa kituo chake kikuu cha kutimiza ajenda yake ya Mashariki ya Kati.

Mike Pompeo besucht König Salman bin Abdul-Aziz in Saudi Arabien
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo,kushoto na mwanamfalme Mohammed Bin Salman wa Saudia, kuliaPicha: picture-alliance/dpa/SPA

Wakati huo huo gazeti linaloiunga mkono serikali ya Uturuki limechapisha taarifa kuhusiana na jinsi Khashoggi alivyouwawa katika ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul mnamo wakati ambapo Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo akiwa amewasili nchini humo leo kwa mazungumzo na Rais Reccep Tayyip Erdogan kuhusiana na kupotea kwa mwandishi huyo.

Pompeo amewasili Uturuki kutoka Riyadh na amesema katika mazungumzo yake na viongozi wa Saudi Arabia hapo jana, viongozi hao walisema kuwa uchunguzi kuhusiana na suala hilo utakuwa wazi.

"Walisema wazi kwamba watauonyesha ulimwengu mzima matokeo ya uchunguzi wao. Walisema pia watamaliza uchunguzi huo kwa haraka, sijui ni lini lakini walisema wanaelewa umuhimu wa kumaliza haraka ili waweze kujibu maswali muhimu," 

Uchunguzi katika makao ya balozi wa Saudia Istanbul umesimamishwa

Huku Pompeo akitazamiwa kufanya mazungumzo huko Uturuki, afisa mmoja wa ngazi ya juu wa nchi hiyo amesema polisi waliokuwa wakichunguza ubalozi mdogo wa Saudi Arabia huko Istanbul walipata ushahidi kwamba Khashoggi aliuwawa katika ubalozi huo.

Türkei Istanbul Konsulat Saudi-Arabien | Untersuchungen Jamal Khashoggi
Ubalozi wa Saudia UturukiPicha: Getty Images/AFP/Y. Akgul

Uturuki kupitia kwa waziri wake wa usalama wa ndani Suleyman Soylu imesema inasubiri makubaliano ya pamoja na Saudi Arabia kufanya uchunguzi katika makao ya balozi wa Saudia mjini Istanbul.

Uchunguzi uliokuwa ukifanywa na maafisa wa Uturuki katika makao hayo umesimamishwa kwa kuwa maafisa wa Saudi Arabia hawakuhusika.

Hayo yakijiri Shirika la Fedha Duniani IMF limesema mkurugenzi wake mkuu Christine Lagarde ameahirisha safari yake kuelekea Mashariki ya Kati. Awali Lagarde alisema kwamba ameshtushwa na kupotea kwa mwandishi wa habari Jamal Khashoggi.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/APE/Reuters

Mhariri: Gakuba Daniel