1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trapp arejea Eintracht Frankfurt

Sekione Kitojo
31 Agosti 2018

Mlinda  mlango  Kevin Trapp amejiunga  tena  na  Eintracht  Frankfurt  kwa makubaliano  ya  mkopo  wa  mwaka  mmoja  kutoka  kwa  mabingwa  wa Ufaransa  Paris Saint-Germain.

https://p.dw.com/p/3478W
Testspiel - Deutschland - Brasilien - Kevin Trapp
Picha: picture-alliance/SvenSimon/J. Kuppert

"Nina  shauku  kubwa  ya  kuuona  mwaka  mwingine nikiwa  na  Frankfurt," alisema  mlinda  mlango  huyo  mwenye  umri  wa  miaka  28 ambaye aliichezea  Eintracht  Frankfurt  kuanzia  mwaka  2012  hadi 2015  kabla  ya kujiunga  na  PSG kwa  kitita  cha  euro  milioni 10.

Kevin Trapp
Mlinda mlango wa Eintracht Frankfurt Kevin TrappPicha: picture-alliance/Revierfoto

Frankfurt ilimpata  Trapp  masaa  kadhaa  kabla  ya  dirisha  la  usajili kufungwa  nchini  Ujerumani  na  Ufaransa  na  atacheza  katika  pambano  la Jumamosi  la  Bundesliga  dhidi  ya  Werder  Bremen.

Trapp, mlinda  mlango  wa  tatu  wa  timu  ya  taifa  ya  Ujerumani  nyuma  ya Manuel Neuer na  Marc-Andre ter Stegen , pia  alijikuta  akiwa  namba  tatu katika  kikosi  cha  PSG nyuma  ya Gianluigi Buffon  na  Alphonse Areola msimu  huu. Alirukia  fursa  ya  kujiunga  na  Frankfurt kwa  msimu  wa  2018 / 19. "Wakati  nilipokuwa  Paris, nilikuwa  nakumbuka  sana  wakati  mzuri nilipokuwa  Frankfurt,"  alisema  Trapp, ambaye  amecheza  mara  tatu  katika lango  la  timu  ya  taifa  ya  Ujerumani  tangu  Juni  2017.

"Mahusiano  hayakuvunjika  na  nilifurahi  sana  wakati  Eintracht iliposhinda kombe  la  Ujerumani, DFB Pokal," aliongeza, akimaanisha  ushindi  wa kushitua  wa  frankfurt  wa  mabao 3-1  dhidi  ya  Bayern  Munich katika  fainali mwezi  Mei  mwaka  huu.

"Ni  muhimu kwangu  mimi  kuwapo  katika  mazingira  ambako  najisikia vizuri na  ambako  naweza  kucheza."

Italien | Ankunft der Fußballnationmannschaft im Trainingslager in Eppan
Kevin Trapp akiwa na mlinda mlango namba moja wa timu ya Ujerumani Manuel Neuer(kulia)Picha: picture-alliance/dpa/C. Charisius

Trapp , ambaye  alikuwa  sehemu  ya  timu  ya  taifa  ya  Ujerumani  katika kombe  la  dunia  ambayo  iliondolewa  na  mapema  katika  awamu  ya makundi, anaweza  kuingia  moja  kwa  moja  katika  kikosi  cha  kwanza  cha Frankfurt  kwa  kuwa  mlinda  mlango  wao  namba  moja  raia  wa  Denmark Frederik Ronnow akiwa  majeruhi baada  ya  kuumia  goti.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Iddi Ssessanga