TOKYO : Koizumi aelekea kushinda uchaguzi mkuu
11 Septemba 2005Serikali ya mseto ya Waziri Mkuu wa Japani inaelekea kushinda katika uchaguzi mkuu wa leo hii ambao umetibuwa ramani ya kisiasa nchini Japani na kuleta matumaini kwamba mageuzi ya kiuchumi yataendelea kuwepo kwenye mkondo.
Koizumi anahitaji ushindi mkubwa kuhakikisha chama chake kilichogawika cha Liberal Demokratik LDP kitaunga mkono agenda yake ya mageuzi kwa kuanzia na ubinafsishaji wa mfumo wa posta wenye thamani kubwa mno ya fedha ambapo mali zake zinafikia dola trilioni 3.
Koizumi mwenye umri wa miaka 63 ameitisha uchaguzi huo wa ghafla baada wabunge wa chama chake cha LDP kuwasaidia wapinzani kuishinda miswada ya kubinafsisha Posta ya Japani katika baraza la juu la bunge.
Uchaguzi huo unaonekana kama kura ya maoni kwa mageuzi ya kiuchumi ya Koizumi na takriban Wajapani milioni 103 wana haki ya kupiga kura.
Uchunguzi wa maoni umetabiri kwamba chama hicho cha Koizumi kitashinda bila ya taabu.