1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tokyo 2020: Mkenya Kipchoge adhibiti taji lake la Marathoni

Zainab Aziz Mhariri: Sudi Mnette
8 Agosti 2021

Mwanariadha wa Kenya Eliud Kipchoge amedhihirisha kuwa mfalme wa mbio za marathoni kwa kulitetea taji lake la Olimpiki nchini Japan. Mashindano hayo yanamalizika leo Jumapili tarehe 8 Agosti.

https://p.dw.com/p/3yhKK
BdTD Berlin Marathon
Picha: Reuters/F. Bensch

Mashindano ya michezo ya Olimpiki Tokyo 2020 yaliyoanza Julai 23 yanakamilika leo Jumapili huko mjini Tokyo, Japan. Licha ya changamoto zilizotokana na maambukizo ya virusi vya corona na joto kali la kupindukia, Wanamichezo wameendelea kuushangaza ulimwengu kwa kuvunja rekodi na kunyakua medali za dhahabu, fedha na shaba katika michuano ya michezo mbalimbali. 

Mwanariadha wa Kenya Eliud Kipchoge amedhihirisha kuwa mfalme wa mbio za marathoni kwa kulitetea taji lake la Olimpiki nchini Japan.

Eliud Kipchoge katika ushindi wake wa mbio za marathoni mnamo Oktoba 12, 2019 mjini Vienna, Austria.
Eliud Kipchoge katika ushindi wake wa mbio za marathoni mnamo Oktoba 12, 2019 mjini Vienna, Austria.Picha: Reuters/L. Foeger

Bingwa huyo amejinyakuliwa medali yake ya dhahabu kwa kukimbia saa 2, dk08 na sek 38. Kwa ushindi huo Kipchoge sasa ameingia katika rekodi za ulimwengu kuwa ni mtu wa tatu tu, kushinda taji hilo kwa mfululizo.

Abdi Nageeye wa Uholanzi amejinyakulia medali ya fedha kwa mbio za saa 2 dakika 9 na sekunde 58 akiwa mbele kidogo ya mwanariadha wa Ubeligiji Bashir Abdi aliyepata medali ya shaba.

Kushoto:Hellen Obiri wa pili kwenye mbio za mita 5000 wanawake Tokyo 2020. Katikati: Mshindi Sifan Hassan wa Uholanzi. Kulia: mshindi wa tatu Gudaf Tsegay wa Ethiopia.
Kushoto:Hellen Obiri wa pili kwenye mbio za mita 5000 wanawake Tokyo 2020. Katikati: Mshindi Sifan Hassan wa Uholanzi. Kulia: mshindi wa tatu Gudaf Tsegay wa Ethiopia.Picha: INA FASSBENDER/AFP

Kipchoge alivunja rekodi kwa tofauti ya dk1 na sek 20 baada ya kuwaacha wapinzani wake kwa umbali mkubwa katika barabara za Sapporo nchini Japan na hatimae kujinyakulia ushindi huo mkubwa tangu mwanariadha Frank Shorter wa Marekani alipotwaa taji hilo katika Michezo ya olimpiki ya mjini Munich, Ujerumani mnamo mwaka 1972.

Ushindi wa mwanariadha huyo wa Kenya Eliud Kipchoge mwenye umri wa miaka 36, ni wa 13 katika jumla ya mashindano ya marathoni 15 alizokimbia tangu mwaka 2013. Kipchoge ametwaa ushindi wake siku moja baada ya mwenzake Peres Jepchirchir kushinda mbio za marathon za wanawake za Tokyo 2020 huku Kenya ikijivunia kunyakua nafasi ya kwanza nay a pili katika mashindano hayo kwenye jiji la Sapporo kaskazini mwa Japan.

Tokio 2020: Mshindi wa mbio za marathoni wanawake Peres Jepchirchir kutoka Kenya.
Tokio 2020: Mshindi wa mbio za marathoni wanawake Peres Jepchirchir kutoka Kenya.Picha: FELINE LIM/REUTERS

Jepchirchir alimshinda mmiliki wa rekodi ya dunia Brigid Kosgei katika hatua za mwisho kushinda katika masaa mawili dakika 27 sekunde 20.

Kipchoge alikuwa na wakimbiaji wenzake Lawrence Cherono na Amos Kipruto waliokimbia kando yake kumpa sapoti.

Majeruhi wawili wa mapema kwenye mbio hizo za marathoni walikuwa Stephen Kiprotich wa Uganda,aliyekuwa mshindi wa medali ya dhahabu kwenye michezo ya London ya mwaka 2012, na bingwa wa ulimwengu huko mjini Moscow, Urusi mwaka mmoja baadaye, na Muethiopia Shura Kitata Tola, mshindi wa Marathon ya London ya mwaka jana ambapo Kipchoge alimaliza wa nane.

Huku Tokyo 2020 ikifikia mukingoni machom yote sasa yanahamia Beijing, China wakati ambapo imebakia miezi sita tu kabla ya kuanza kwa michezo ya msimu wa baridi. Hali sio shwari sana kwani miito ya kuisusia michezo hiyo inazidi kupamba moto kutokana na maambukizi ya virusi vya corona

Wakati huo huo China itakuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpiki ambayo imepangiwa kufanyika kuanzia Februari 4 hadi 20, mwaka 2022. Mji mkuu wa China, Beijing utakuwa ni jiji la kwanza kuandaa michezo ya misimu wa baridi na joto.

Vyanzo:AP/AFP