1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Timu zilizopanda daraja Bundesliga ziko hoi

21 Agosti 2023

Timu zilizopandishwa daraja msimu huu Heidenheim na Darmstadt zimekuwa na mwanzo mbaya wa Ligi Kuu ya Ujerumani baada ya kupokea kichapo mwishoni mwa wiki katika mechi zao za kwanza.

https://p.dw.com/p/4VPU2
Kandanda Bundesliga | VfL Wolfsburg - 1. FC Heidenheim
Adrian Beck wa Heidenheim (kushoto) akipigania mpira na Mattias Svanberg wa WolfsburgPicha: Swen Pförtner/dpa/picture alliance

Darmstadt walikuwa ugenini mjini Frankfurt wakipambana na wenyeji Eintracht Frankfurt na walinyamazishwa 1-0. Randal Kolo Muani ndiye aliyekuwa mfungaji wa goli hilo la pekee kunako dakika ya 40.

Heidenheim wao walikuwa wamewatembelea VfL Wolfsburg na wakalemazwa 2-0 Jonas Wind aking'ara sana katika mpambano huo kwa kufunga mabao yote mawili.

Kocha wa Bayer Leverkusen Xabi Alonso alianzia pale alipoachia msimu uliopita kwa kupata ushindi katika mojawapo ya mechi kubwa za Bundesliga, baada ya vijana wake waliokuwa katika udongo wa nyumbani kuwacharaza RB Leipzig 3-2.

Bayer Leverkusen - RB Leipzig
Wachezaji wa Bayer Leverkusen wakisherehekea bao dhidi ya RB LeipzigPicha: Marius Becker/dpa/picture alliance

Leverkusen waliokuwa nyumbani walifungiwa mabao yao na jeremie Frimpong, Jonathan Tah na Florian Wirtz kisha Leipzig wakapata magoli kupitia kwa Dani Olmo na mchezaji wao mpya Lois Openda.

Borussia Dortmund walipata ushindi mwembamba wa 1-0 walipokuwa wenyeji wa majirani zao FC Köln, Donyell Malen akiwa mfungaji wa goli hilo la pekee.

Chanzo: DPAE/APE/Reuters