1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theresa May kukutana na viongozi wa Ulaya kuzungumzia Brexit

11 Desemba 2018

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amezindua upya vita vyake vya kuokoa mpango wake wa kutaka Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya, unaojulikana kama Brexit, wakati alipokutana na mwenzake wa Uholanzi Mark Rutte.

https://p.dw.com/p/39qSe
Niederlande Theresa May, Premierministerin Großbritannien & Mark Rutte
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May na mwenzake wa Uholanzi Mark Rutte alipowasili mjini The HaguePicha: picture-alliance/AP Photo/P. Dejong

Mkutano huo kati ya May na Rutte ndio wa kwanza miongoni mwa mikutano anayotarajiwa kufanywa na viongozi wa Ulaya katika siku zijazo. May aliwasili katika makazi ya Rutte mapema leo mjini The Hague na baadaye anatarajiwa kuelekea Berlin na Brussels.

Ziara ya May inajiri siku ambayo wabunge wa Uingereza walitarajiwa kuupigia kura mpango huo. May atatafuta hakikisho zaidi na kuurejesha mpango huo bungeni kwa mashauriano zaidi. Mpango wa bi May wa kujiondoa Umoja wa Ulaya - kwa kiasi kikubwa ulitarajiwa kukataliwa na wabunge wengi ikiwemo wa chama chake.

May verschiebt Brexit-Abstimmung
Picha: picture alliance/empics

Katika hotuba yake bungeni jana aliutetea mpango wake huo akisema ni njia pekee ya kuwahakikisha waingereza hadhi yao. May alisema,"Ni wazi kwamba licha ya kuwa baadhi ya masuala mengi ya mpango huu yanaungwa mkono, kuhusu suala moja linalohusu Ireland ya Kaskazini, bado kuna wasiwasi wa hali ya juu. Matokeo yake yatakuwa iwapo tutaandaa kura mpango huu utakataliwa kwa kiasi kikubwa. Hivyo tutaahirisha kura hiyo na hatutaendelea kuligawanya bunge zaidi kwa wakati huu."

Hayo yakijiri, mbunge mmoja mkosoaji katika chama cha May cha Conservative ameliambia shirika la habari la BBC leo kwamba nafasi ya May inafaa kuchukuliwa na mtu mwingine huku akiwaomba wenzake kuitisha kura ya kutokuwa na imani na uongozi wake. Aidha ameongeza kuwa iwapo hawawezi kuendelea na mpango wa May, ana wasiwasi kwamba njia ya kipekee ya kubadili sera ni kumbadilisha Waziri Mkuu, na kwamba anafikiri ni jukumu lake kuondoka.

Iralnd Simon Coveney
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland Simon CoveneyPicha: picture-alliance/empics/K. O'Connor

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland Simon Coveney leo anatarajiwa kuwasilisha waraka wa kina bungeni kuhusu maandalizi ya matukio mbalimbali ya Brexit, ikiwemo Uingereza kujiondoa bila makubaliano yoyote, hatua anayosema serikali inafaa kujiandaa nayo.

Kadhalika amesema kwa sasa si kujiandaa tu kwa hilo, lakini kuchukua hatua kuhakikisha kwamba iwapo kutakuwa na haja watakuwa tayari tarehe 29 mwezi Machi mwaka ujao kwa Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya bila makubaliano. Ikumbukwe mapema jana, msemaji wa Tume ya Ulaya Jean Claude Junker, alisema kwamba mkataba walioutoa ndio bora na kwamba hawawezi kuujadili tena.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/RTRE/APE

Mhariri: Josephat Charo