1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theresa May azidi kuzongwa kuhusu Brexit

Sekione Kitojo
16 Novemba 2018

Waziri  mkuu  Theresa  May amepambana  leo Ijumaa(16.11.2018) kuokoa mswada  wa  makubaliano  ya Brexit  wa kujitoa  kutoka Umoja  wa Ulaya pamoja  na  hali  yake  ya  baadae  ya kisiasa.

https://p.dw.com/p/38Mm1
Großbritannien Theresa May in London
Picha: picture-alliance/dpa/M. Dunham

Baada  ya siku  ya  jana  iliyokuwa na vurumai  ambapo  mawaziri  walijiuzulu na   wanachama  wa  chama  chake  kupanga  njama  za  kumuondoa madarakani, May  alikabiliana  na  umma  kutetea  msimamo  wake , katika  kipindi  cha  redio  ambamo  watu  walipiga  simu  kumuuliza maswali.

Theresa May
Theresa May waziri mkuu wa UingerezaPicha: picture-alliance/empics

Kiongozi  huyo  wa  chama  cha  Conservative  alisema  kuwa anaamini  kila  sehemu  ya  mwili  wake  kuhusu  mwelekeo  wa Brexit ambao  ameupanga, baada  ya  kukabiliana  na  bunge hasimu  na  kushuhudia  mawaziri  wanne , ikiwa  ni  pamoja  na waziri  anayehusika  na  Brexit  Dominic Raab, wakijitoa  kutoka katika  serikali  yake. Wabunge kutoka  pande  zote  walimuonya kwamba  hakuna uwezekano  wowote  ambapo  mpango  wake unaweza  kupata  uungwaji  wao  mkono, lakini  alipuuzia  miito  ya kutaka  ajiuzulu, akisema, "nitahakikisha  hili  linafika  mwisho".

Waziri  mkuu  amekiri  kuwapo  na "wasiwasi  kuhusu suluhisho  la muda  mfupi " kuhusiana  na  suala  la mpaka  na  Ireland  katika makubaliano  hayo, ambapo  wanaounga  mkono  Brexit  wanahofu litaifunga Uingereza  bila  ukomo  katika  umoja  wa  forodha.

EU Brexitabkommen vorgestellt
Mkuu wa majadiliano ya Brexit wa Umoja wa Ulaya Michel Barnier akutana na rais wa baraza la Ulaya Donald Tusk kuwasilisha makubaliano kati ya Uingereza na Umoja huoPicha: Reuters/F. Lenoir

Kura ya pili ya maoni

Wakosoaji  wanaamini  May  amekubaliana katika  mambo  mengi na  Umoja  wa  Ulaya   katika  maeneo  muhimu, wakati  waounga mkono  kubakia  katika  Umoja  wa  Ulaya  wanatoa  wito  wa kufanyika  kura  ya  pili  ya  maoni kuhusu  makubaliano  ya  mwisho.

"Nimechukua  mtazamo  wa  wazi  juu  ya  suala  la  kura  ya  maoni ya  pili, nimeweka  wazi  kwa  wabunge. Na  nafikiri  wengi  wa wabunge  wanatambua  wamewapa fursa  wananchi  wa  Uingereza kupiga  kura  na  wananchi  wameamua, ni  juu  yetu  kutimiza kuhusu  kura  hiyo na  sio  kura  ya  pili  ya  maoni. Kwa kadiri ninavyoamini, hakutakuwa  na  kura  ya  pili  ya  maoni."

Waziri  wa  mazingira Michael Gove, mmoja  kati  ya  watu  muhimu katika  kampeni  ya  kuunga  mkono  Brexit  katika  kura  ya  maoni ya  mwaka  2016 kuhusiana  na  uanachama  wa  Uingereza  katika Umoja  wa  Ulaya , alikataa  ombi  la  kuchukua  nafasi  ya  Dominic Raab  na  anatafakari  kuhusu  msimamo  wake, kwa  mujibu wa ripoti  za vyombo  kadhaa  vya  habari.

Großbritanien Kabinett May Michael Gove
Michael Gove, waziri wa sheria wa UingerezaPicha: imago/i Images/M. Thomas

Mamia  kadhaa  ya  watu  waliandamana  nje  ya  bunge  mjini London  jana  wakidai  kufanyika  kura  ya  pili  ya  maoni  kuhusu Brexit .

Waandamanaji , wengi  wao kutoka  chama  cha  siasa  za  wastani kinachopendelea  kubakia  katika  Umoja  wa  Ulaya  cha  Liberal Democrats kimeeleza  kutoridhishwa  na  mswada  wa  makubaliano yaliyofikiwa  kati ya  waziri  mkuu  May  na  Umoja  wa  Ulaya  katika masharti ya  Uingereza  kujitoa  kutoka  Umoja  huo. Nacho  chama cha  Ireland  ya  kaskazini  cha  Democratic Unionist , ambacho wabunge  wake  10 wamemsaidia  May kuwa  na  wingi  mdogo bungeni , kinasema kitapiga kura  dhidi  ya  makubaliano  hayo.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman