1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theresa May ataka kubadilisha makubaliano ya Brexit

30 Januari 2019

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May, anajiandaa kurudi kwenye Umoja wa Ulaya katika jitihada za kujadili tena vipengele muhimu vya mpango wake kuhusu mchakato wa Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya-Brexit.

https://p.dw.com/p/3CPdQ
Großbritannien House of Commons in London | Theresa May, Premierministerin
Picha: picture-alliance/House of Commons/empics

Wabunge wa Uingereza siku ya Jumanne walipiga kura juu ya mapendekezo saba yaliyochaguliwa na spika wa bunge yaliyolenga kuleta mabadiliko katika mchakato wa Brexit. Wabunge hao walipitisha mabadiliko yanayoitaka serikali kuepusha uwezekano wa Uingereza kuondoka Umoja wa Ulaya bila ya mkataba ifikapo Machi 29. 

Lakini ishara zote zinaonyesha kwamba waziri mkuu wa Uingereza anaelekea katika malumbano mapya na Umoja wa Ulaya baada ya kuahidi kubadili makubaliano yaliyokwisha kufikiwa kuhusiana na mchakato wa Brexit, mpango aliotumia muda wa mwaka mmoja na nusu kujadiliana na nchi za Umoja wa Ulaya.

Katika kujaribu kuyafufua mazungumzo ya Brexit yaliyokwama, May amepewa jukumu na bunge la nchi yake la kurudi kwenye makao makuu ya Umoja wa Ulaya ili kuuzungumzia tena mkataba uliopo sasa juu Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya.

May anapanga kujadili na Umoja wa Ulaya juu ya kipengele kinachohusu suala lenye utata la mpaka wa Ireland kilichokwisha kutiwa saini na nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya ambacho sasa Uingereza inataka kibadilishwe.

Wabunge wa Uingereza wakisubiri kuyapigia kura mapendekezo mapya juu ya Brexit
Wabunge wa Uingereza wakisubiri kuyapigia kura mapendekezo mapya juu ya BrexitPicha: picture-alliance/empics

Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya wamesisitiza kuwa kipengele hicho hakiwezi kubadilishwa. Msemaji wa rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk amesema suala hilo la mpaka wa Ireland ni sehemu ya mkataba juu ya Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya na kwamba haliwezi kujadiliwa upya. Akizungumza baada ya bunge la Uingereza kupiga kura May alisema:

Tangu serikali ya May ifikie makubaliano yaliyopo sasa ya mpango wa Brexit na Umoja wa Ulaya mwaka jana, waziri mkuu huyo amekabiliwa amekuwa na matatizo kuufanya mpango wake ukubalike na wabunge wa Uingereza, ikiwa ni pamoja na wabunge kadhaa ndani ya chama chake. Mapema mwezi huu, bunge la Uingereza liliukataa mpango huo ulioshindwa bungeni kwa karibu na theluthi mbili ya kura zilizopigwa.

Binafsi waziri mkuu May anatambua kuwa Umoja wa Ulaya hauna hamu wala hautaki kuubadilisha mpango wa Brexit uliopo sasa, lakini imeahidi kwenda mjini Brussels na kutafuta mabadiliko makubwa na ya kisheria kuhusu mkataba wa Brexit. May ameahidi kujadiliana tena kuhusu mpango wake wa Brexit ama kurudi bungeni mnamo Februaari 13 ili mustakabali mpya wa mpango wa Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya upigiwe kura.

Lakini wachambuzi wanasema hatua hiyo inaweza kuwa na mafanikio madogo sana na iliyo chelewa mno huku mkataba ukiwa bado haujapatikana na bila dalili zozote kuonekana kwamba utapatikana hivi karibuni, wakati ambapo 29 Machi inakaribia siku ambayo Uingereza inatakiwa kuondoka kutoka Umoja wa Ulaya!

Mwandishi:Zainab Aziz/AFPE/p.dw.com/p/3CPOO

Mhariri:Caro Robi