1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

THE HAGUE: Uholanzi kutoa yuro milioni 4.5

1 Agosti 2006
https://p.dw.com/p/CDPt

Wizara ya mambo ya kigeni nchini Uholanzi imesema nchi hiyo itatoa kiasi cha yuro milioni 4.5 kwa mashirika ya kutoa misaada ya kiutu yanayotoa huduma nchini Lebanon.

Katika taarifa yake serikali imesema shirika la msalaba mwekundu litapokea yuro milioni 1.5 juu ya kiwango cha yuro milioni moja zilizoahidiwa shirika hilo wiki iliyopita.

Fedha hizo zitatumiwa kugharimia matibabu, kuwasaidia watu wasio na makao, kununulia chakula, mablanketi, maji safi na vyombo vya kupikia.

Shirika la chakula duniani, WFP, litapewa yuro milioni 1.5. Uholanzi pia imeahidi kuyasaidia mashirika ya misaada yanayofanya kazi katika Ukanda wa Gaza na nchini Syria.

Shirika la WFP limetangaza leo kwamba magari yake ya misaada yamewasili katika kijiji cha Qana, kusini mwa Lebanon, ingawa misafara miwili ya magari imezuiliwa na jeshi la Israel.

Kiwango kitakochotolewa na Uholanzi kwa ujumla ni yuro milioni 6.3 tangu mapigano kati ya Israel na kundi la Hezbollah yalipoanza wiki tatu zilizopita.