1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tetemeko lawauwa watu 91 Indonesia

6 Agosti 2018

Takribani watu 91 wamekufa kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililopiga kisiwa cha utalii cha Lombok nchini Indonesia, na kukitikisa kisiwa jirani cha Bali.

https://p.dw.com/p/32fuM
Indonesien nach dem Erdbeben in Lombok zertörte Häuser
Picha: Reuters/Antara Foto/A. Subaidi

Serikali ya Indonesia imesema Jumatatu kwamba kikosi cha uokozi bado hakijafanikiwa kuyafikia maeneo yaliyoathirika zaidi na huenda idadi ya vifo ikaongezeka.

Waziri wa jimbo la Nusa Tenggara Magharibi Rosiady Sayuti, amekiambia kituo cha televisheni cha Metro kwamba watu 142 wamekufa kutokana na tetemeko hilo. Amesema nyumba nyingi ziliharibiwa kabisa. Hata hivyo msemaji wa taasisi ya kitaifa inayoshughulikia majanga Sutopo Nughoro amekataa kuthibitisha taarifa hiyo. Amesisitiza kwamba idadi rasmi ya vifo hivyo ni 91, lakini akiongeza kwamba inaweza kuongezeka.

Kumekuwa na uharibifu mkubwa mno

Hili ni tetemeko la pili  kubwa kutokea katika kipindi cha wiki moja kwenye kisiwa hicho cha Lombok. Tetemeko jingine lililotokea Julai 29 lilisababisha vifo vya watu 16 na kuharibu mamia ya makazi, ambayo miongoni mwake yalianguka na kuua watu waliokuwemo ndani.

Indonesien nach dem Erdbeben in Lombok
Uharibifu uliotokana na tetemeko la ardhi IndonesiaPicha: picture-alliance/AA/J. Delita

Msemaji wa taasisi ya kitaifa inayoshughulikia majanga Sutopo Purwo Nugroho ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba kumekuwa na uharibifu mkubwa katika eneo la kaskazini mwa Lombok, na baadhi ya maeneo hayafikiki kwa urahisi, na kuongeza kuwa hadi sasa wengi wa wahanga wa tetemeko hilo ni raia wa Indonesia.

"Wengi wamekufa baada ya kuangukiwa na majengo. Idadi hiyo ya watu 91 waliokufa ni raia wa Indonesia. Hadi wakati huu hatujaweza kupata taarifa ya wahanga ambao ni raia wa kigeni waliopo Bali ama katika jimbo la Nusa Tenggara magharibi," alisema msemaji huyo.

Baadhi ya maeneo hayafikiki kwa urahisi kwa kuwa barabara zimezuiwa na vifusi, kukatika kwa umeme na madaraja yameanguka.

Sutopo amesema idadi ya vifo imepanda hadi 91 na zaidi ya watu 200 walikuwa wamejeruhiwa vibaya. Maelfu ya makazi na majengo yameharibiwa na watu 20,000 wamejihifadhi katika makazi ya muda.

Maelfu ya watalii walilazimika kulala nje

Tetemeko hilo la kipimo cha 7.0, hii ikiwa ni kulingana na mamlaka za Indonesia, lilipiga kisiwa hicho jioni ya jana Jumapili katika eneo la kaskazini mwa Lombok, na kusababisha kutolewa onyo la kimbunga cha Tsunami, lilisababisha watu kutoka nje ya nyumba zao na kukimbilia kwenye maeneo yaliyo na miinuko, na hasa katika eneo la kaskazini mwa Lombok na Mataram, ambako ni mji mkuu wa jimbo la Nusa Tenngara Magharibi. Hata hivyo onyo hilo liliondolewa baadaye.

Indonesien nach dem Erdbeben in Lombok
Wahanga wa tetemeko la ardhi wakiwa nje ya hospitali Picha: Reuters/J. P. Christo

Katika moja ya visiwa maarufu vya utalii karibu na Lombok, maelfu ya watalii wa nje na wa ndani walilazimika kulala milimani wakohofia tsunami, wamethibitisha watalii kutoka Uingereza na Marekani.

Maelfu ya wakazi walioshikwa na uwoga, hivi sasa wanajaribu kuondoka kwenye kisiwa hicho. Kulingana na Nugroho, hakuna raia wa kigeni aliyejeruhiwa, miongoni mwa watalii wa nje na wa ndani na kikosi cha pamoja cha uokozi kimepeleka meli tatu kuwaokoa watu.

Mwandishi: Lilian Mtono/DPAE/APE

Mhariri: Daniel Gakuba