Tetemeko la ardhi lawaua takriban watu 400 Indonesia
29 Septemba 2018Shirika la kitaifa la kukabiliana na mikasa na majanga limesema watu 384 wameuawa na tetemeko hilo, karibu wote kutoka mji wa Palu, lakini limeonya kuwa idadi ya waathiriwa inatarajiwa kuongezeka.
Mji wa Palu una wakazi karibu 350,000 na shirika la kukabiliana na mikasa na majanga la Indonesia limesema mamia ya watu waliokuwa wakijiandaa kwa tamasha iliyopaswa kufanyika katika fukwe za kisiwa hicho siku ya Ijumaa hawajulikani waliko.
Mamia wamejeruhiwa
Hospitali zimefurika watu waliopata majera, wengi wao wakitibiwa nje ya hospitali kutokana na kwamba hospitali haziwezi kuwapokea wagonjwa zaidi.
Tsunami hiyo iliyokikumba kisiwa hicho cha Sulawesi, ilitokana na tetemeko kubwa la ardhi lililoyaporomosha majengo kadhaa mjini Palu na kusababisha wakaazi wa mji huo kukimbilia nyanda za juu.
Barabara hazipitiki, uwanja wa ndege wa Palu umefungwa kwa kipindi cha saa 24 zijazo na huduma za umeme, pia zimekatika kutokana na athari ya tetemeko hilo la ukubwa wa 7.5 kulingana na vipimo vya Ritcher.
Rais wa Indonesia Joko Widodo amesema jeshi limeagizwa kwenda katika eneo la mkasa kusaidia maafisa wa ukozi kupata majeruhi na kupata miili ya waliofariki.
Indonesia ni mojawapo ya nchi zinazokumbwa na majanga ya kimazingira ya mara kwa mara duniani. Mapema mwaka huu, tetemeko kubwa la ardhi lilikikumba kisiwa cha Lombok na kisiwa jirani cha Sumatra na kuwaua watu 550.
Mnamo mwaka 2004 tetemeko jingine la ardhi liliwaua watu 168,000 nchini humo. Mnamo mwaka 2010, karibu watu 430 waliuawa wakati tetemeko la ardhi lilipokunmba eneo la pwani la Sumatra na wengine 600 waliuawa katika kisiwa cha Java.
Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters/dpa
Mhariri: Zainab Aziz-Mtullya