1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TEHRAN:Iran yazionya Marekani na Umoja wa Ulaya dhidi ya mpango wake wa Nuklia

11 Agosti 2005
https://p.dw.com/p/CEm3

Iran imezionya Marekani na Umoja wa Ulaya dhidi ya kuifikisha nchi hiyo mbele ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa juu ya mpango wake wa Nuklia.

Onyo hilo limetolewa na Iran baada ya kuviondosha vizuizi vyote vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa kwenye mtambo wake wa kurutubisha madini ya Uranium wa Isfahan na kuufanya mtambo huo kuanza kazi kikamilifu.

Hatua ya Iran imezusha hofu kwa mataifa ya magharibi ambayo yanadai huenda nchi hiyo ikayatumia madini hayo kutengeneza bomu la Nuklia.

Umoja wa Ulaya umewasilisha azimio kwa shirika la kudhibiti matumizi ya nguvu za Atomiki duniani la kuitolea mwito Iran ikomeshe shughuli zake nyeti za Nuklia.

Maofisa wa shirika hilo wamekubaliana na ombi la Iran la kuviondosha vizuizi baada ya kuwekwa kamera za kunasa shughuli zinazoendelea kwenye mtambo huo ili kuhakikisha kwamba mtambo huo hautumiwi kutengeneza silaha za Nuklia.

Ujerumani imeitolea mwito Iran kuufikiria tena uamuzi wake wa kukataa mapendekezo ya Umoja wa Ulaya.