1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TDF watwaa udhibiti wa Tigray, Ethiopia yakiri vifo vingi

30 Juni 2021

Wakati wapiganaji wa chama cha TPLF wakiendelea kuchukuwa udhibiti wa maeneo kadhaa muhimu ya jimbo la Tigray, serikali ya Ethiopia imekiri kwamba wanajeshi na raia wengi wameuawa kwenye jimbo hilo la kaskazini.

https://p.dw.com/p/3voT3
Äthiopien I Konfliktregion Tigray
Picha: Ethiopian News Agency/AP/picture alliance

Katika kile kinachotazamwa kama kauli ya kwanza kutolewa na afisa wa juu wa Ethiopia tangu mji mkuu wa Tigray, Mekelle, kutwaliwa na vikosi vya TDF - tawi la kijeshi la chama cha TPLF kilichokuwa kinatawala jimbo hilo, msemaji wa serikali kwa ajili ya jimbo hilo, Redwan Hussein, alisema siku ya Jumatano (Juni 30) kwamba wanajeshi na raia wengi walipoteza maisha kwenye mapigano kati ya jeshi la shirikisho na wapiganaji wa TDF, akiongeza kwamba "kwa sababu ya vita hivyo, sasa Ethiopia nzima iko hatarini kushambuliwa na watu kutoka nje." 

Msemaji huyo aliwaambia waandishi wa habari kuwa hiyo ndiyo sababu pekee ya uamuzi wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed kuamuru kusitishwa mapigano mara moja na bila masharti yoyote siku ya Jumatatu (Juni 28).

Hata hivyo, msemaji wa chama cha TPLF, Getachaw Reda, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba tangazo hilo la kusitisha mapigano lilikuwa "mzaha mtupu", akisisitiza kwamba wapiganaji wao walikuwa wako njiani kulikomboa jimbo zima kutoka mikono ya wale aliowaita "wavamizi na maadui".

Ripoti kutoka Tigray zilithibitisha kwamba jeshi la TDF lilifanikiwa kuyatwaa maeneo mengi ya jimbo hilo. Chanzo kimoja kutoka Umoja wa Mataifa kilisema kuwa wapiganaji hao wameingia kwenye mji wa Shire ulio umbali wa kilomita 140 kutoka Mekelle. 

Wanajeshi wa Ethiopia, Eritrea 'watoweka'

Bildergalerie Äthiopien | Flucht aus der Region Tigray
Wanajeshi wa Ethiopia wakiondoka Tigray.Picha: Baz Ratner/REUTERS

Shirika la habari la AFP liliripoti kuwepo kwa makundi ya watu wanaosherehekea ushindi wa TDF kwenye mitaa ya miji kadhaa mikubwa, huku  wanajeshi wa serikali ya shirikisho, washirika wao wa Eritrea na viongozi wa serikali walioteuliwa na Waziri Mkuu Abiy Ahmed wakivikimbia vituo vyao.

Taarifa iliyotolewa usiku wa Jumanne (Juni 29) na serikali ya jimbo la Tigray iliyokuwapo kabla ya vita ililipongeza jeshi wa TDF kwa kusonga mbele na kuwataka wapiganaji wake kuongeza mashambulizi zaidi.

"Serikali ya Tigray inawatolea wito watu na jeshi la Tigray kuongeza mapambano hadi maadui wetu wawe wameondoka kikamilifu Tigray." Ilisema taarifa hiyo.

Shirika la International Crisis Group lilisema kwamba TDF sasa ilikuwa inadhibiiti sehemu kubwa ya jimbo hilo, ikiwemo miji yote mikubwa.

Kwa mujibu wa mchambuzi wa ngazi za juu wa shirika hilo, William Davison, mafanikio hayo yalitokana na "kuungwa mkono na umma na kukamata shehena za silaha, bidhaa na vifaa vya maadui zao."