1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yakiri upungufu wa ajira na tofauti ya kipato

29 Juni 2021

Tanzania imesema inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo utofauti wa kiwango cha kipato na uwezo mdogo wa watu kukidhi mahitaji yao ya msingi, upungufu wa ajira za uhakika na hali ya mabadiliko ya tabia ya nchi.

https://p.dw.com/p/3vlIm
Kassim Majaliwa, Premierminister von Tansania
Picha: Büro des Premierministers von Tansania

Aidha, serikali ya Tanzania imesema pia imeweka hadharani idadi ya wagonjwa wa COVID-19 kufuatia wimbi la tatu la janga hilo linaloisumbua dunia hivi sasa.

Kauli hiyo ya serikali ya Tanzania imetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wakati akizindua mpango wa tatu wa maendeleo wa taifa wa miaka mitano mwaka 2021/2024 jijini Dodoma.

COVID-19 moja ya changamoto

Majaliwa amesema kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana katika mpango wa pili wa maendeleo, bado Tanzania imeendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali zinazosababishwa na mambo kadha wa kadha ikiwemo janga la virusi vya corona.

Wakati janga la Covid-19 likielezwa kuwa ni miongoni mwa sababu zilizochangia Tanzania kukabiliwa na changamoto mbalimbali zinazotatiza ukuaji wa maendeleo kiuchumi, tayari serikali ya nchi hiyo imeweka hadharani kuwa inakabiliwa na wimbi la tatu la virusi vya corona, huku ikiwasisitiza wananchi kufuata taratibu zote zinazotolewa na wataalam wa afya.

Tansania l Neue Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu HassanPicha: AP/picture alliance

Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari siku ya Jumatatu, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, alisema kufuatia kuwepo na wimbi hilo la tatu virusi vya corona tayari amekutana na baraza lake la mawaziri kuijadili ripoti ya kamati ya wataalam wa afya aliyoiunda baada ya kuona wimbi la pili lilivyoipiga Tanzania.

Rais Samia aliongeza kusema kuwa hatua zilizochukuliwa na serikali yake ili kupambana na wimbi hilo la tatu la virusi vya corona ni pamoja na kukubali dunia inavyotaka kwenda ikiwemo kuruhusu chanjo huku Rais Samia akisistiza kuwa chanjo hiyo itakuwa ni hiari ya mtu kuchanjwa.

Wimbi la kwanza la mripuko wa virusi vya corona liliiathiri Tanzania sio kwa kiasi kikubwa kutokana tahadhari za kiafya zilizochukulia, tofauti na hivi sasa inavyoelezwa wimbi la pili kuacha athari kubwa.