1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiTanzania

Tanzania yakabiliwa na upungufu wa fedha za kigeni

19 Februari 2024

nchini Tanzania kunashuhudiwa upungufu mkubwa wa fedha za kigeni, hasa dola ya Marekani, ambayo ni muhimu kwa biashara ya kimataifa na pia kwa watu wanaotajia kwenda kuhiji mwaka huu

https://p.dw.com/p/4caGl
Dola ya Marekani ikihesabiwa
Dola ya Marekani ikihesabiwaPicha: Khaled Elfiqi/epa/dpa/picture alliance

Katika jitihada za kukabiliana na upungufu huo wa fedha za kigeni, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inasema itarejesha huduma za kubadilishia fedha kwa maduka binafsi badala ya benki peke yake, ili kukusanya fedha ambazo hazimo katika mfumo rasmi na kuziingiza katika mfumo rasmi ya taasisi za kifedha yakiwemo mabenki. 

Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania, uhaba unaoshuhudiwa sasa wa fedha za kigeni unatokana na hali ya mtikisiko wa uchumi uliosababishwa na vita vya Ukreine na Urusi, janga la UVIKO-19na machafuko ya Mashariki ya Kati.

John Mero ni meneja msaidizi masuala ya fedha wa Benki hiyo anakiri taifa hilo la Afrika mashariki kukumbwa na uhaba wa fedha, akiunganisha na changamoto za kiuchumi ambazo dunia sasa inapitia.

"Tulikumbwa na changamoto ya uhaba wa fedha za kigeni, lakini pia hii ni kutokana na mgogoro ya kisiasa ambayo dunia inapitia ikiwemo mashariki ya Kati na Ukraine" Alisema Mero.

Soma pia:Kenya yakabiliwa na upungufu wa sarafu ya dola

Mbali ya sababu hizo, kitu chengine kinachotajwa kuchangia upungufu uliopo sasa wa fedha za kigeni ni hatua ya kufungwa kwa maduka ya kubadilishia fedha iliyochukuliwa  na awamu iliyopita ya uongozi wa nchi.

Baadhi ya wafanyabishara ya ubadilishaji fedha wanasema kuwa fedha za kigeni zipo mtaani hasa dola lakini kutokana na ushindani wa biashara kuwa finyu baduka yalioidhinishwa kufanya biashara hiyo yanakabiliwa na uhaba mkubwa.

"Sio kama dola haipo, ipo na tunaushahidi sababu wateja wanapokuja wanalinganisha bei na maduka ya mtaani" Faraji Juma ambae ni mbadilishaji wa fedha za kigeni alisema.

Mahujaji wakabiliwa na changamoto ya fedha za kigeni

Mbali na biashara nyengine za kimataifa zinazofanyika hapa nchini, fedha hizo za kigeni zinahitajika zaidi katika kipindi hiki ambacho Waislamu wanajiandaa kwa ajili ya kutekeleza nguzo ya tano ya Uislamu ya kwenda Hija ambapo waandaaji wa safari hizo wamekiri kuwepo kwa ugumu wa upatikanaji wa fedha.

Serikali ya Tanzania ilipoteza shilingi trilioni 1.5?

Badru Adam ni mwenyekiti wa Zanzibar Hajj anasema dola imeadimika kwa kiwango kikubwa na kusababisha wale wanaouza nje ya mfumo rasmi kubadili bei katika mtindo ambao unaumiza wanunuzi.

"Mahujaji wamekuwa wakipata changamoto, kwa sasa dola inauzwa hadi 2,800, kwenye soko la magendo."

Soma pia:Sarafu ya Uingereza yaanguka dhidi ya dola

Wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa kutoka nje ya nchi wanalalamikia upungufu wa dola, ambao umesababisha mfumko wa bei na kupanda kwa gharama za maisha, ambako kumezuwa malalamiko mengi miongoni mwa wananchi. 

Licha ya kukiri kuwepo kwa upungufu wa fedha za kigeni, bado kupitia Benki Kuu ya Tanzania, serikali inasema hali haijawa mbaya ikilinganishwa na nchi jirani, kwani Tanzania bado ina fedha za kutosha. Mtafiti msaidizi wa BoT, Dkt. Lusajo Mwakemwa: