1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yafungua akaunti za watetezi wa Haki za Binadamu

21 Aprili 2021

Mtandao wa haki za binadamu nchini Tanzania umetangaza kufunguliwa kwa akaunti zake za benki ambazo zilifungiwa kwa kipindi cha miezi nane ili kuchunguza uhalali wa miamala iliotajwa kufululiza katika akaunti hizo, hatua iliosababisha shughuli za mtandao huo kuzorota kwa kiwango kikubwa.

https://p.dw.com/p/3sJxA

Kufunguliwa kwa akaunti hizo kunatokana na maelekezo ya mamlaka za serikali zilizoagiza kufungwa kwa akaunti hizo, ili kufanya uchunguzi dhidi ya miamala ilioingia kwenye akaunti ya asasi hiyo inayojihusissha na masuala ya utetezi wa haki za binadamu.

Mkuu wa jeshi la polisi nchini Simon Sirro aliwahi kunukuliwa akisema, jeshi la polisi kitengo cha ufuatiliaji wa fedha haramu kilifuatilia mwenendo wa miamala katika akaunti za mtandao huo tangu mwaka 2019 hadi August mwaka 2020 na kubaini kuingia kwa fedha takriban shilingi bilioni 6, hivyo walizifunga ili kujua uhalali wake kama sheria inavyowaelekeza.

Vicy Ntentema mwandishi habari na mwanaharakati wa haki za binadamu kwenye mtandao huo amesema kufungwa kwa akaunti hizo kulisababisha kuyumba kwa utendaji wa majukumu ya mtandao hasa kwenye miradi ya kutetea haki za binadam, kama ambavyo walikuwa wamejiainishia kwenye mipango ya taasisi hiyo kwa mwaka wa 2020, ukizingatia wakati huo taifa lilikuwa katika uchaguzi.

Mtandao wa Haki za Binadamu kuendelea na kazi bila hofu 

Tansania Kinderhochzeit Kinder Ehe Afrika Menschenrechte
Miradi ya watetezi wa haki za binadamu ni muhimu kusaidia wananchi kupata hakiPicha: Zuberi Mussa

Aidha mtandao huo umeahidi kuendelea kutekeleza majukumu yake bila hofu, bali kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa na mamlaka zote, ili kuhakikisha kuwa utetezi wa haki za binadamu unaendelea kutamalakai katika taifa hilo ambalo hivi karibuni katika taasisi za kimataifa zinazoangalia utekelezwaji wa haki za binadamu lilitajwa kuporomoka kwa kiwango kikubwa.

Itakumbukwa kuwa, wiki chache zilizopita mwenyekiti wa chama cha upinzani pia nae alitoka hadharani ambapo mbali na mambo mengi alitaja kufunguliwa kwa akaunti zake ambazo zilikuwa zimefungwa na mamlaka kutokana na sababu mbalimbali.

Wafuatiliaji wa mambo hapa nchini naizungumzia hatua hii kama mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan Katika kutekeleza azma yake ya kuleta maridhiano ya kitaifa kwa vitendo, lakini wanasema haitoshi na kuna haja ya kubadili mfumo ikiwemo sheria ambazo zilitoa mwanya kufanikisha hayo.

Baadhi ya watu ambao walikuwa wananufaika na mtandao huo wa haki za binadamu, wamefurahishwa na hatua hiyo ya mamalaka kwa hoja kuwa, wataweza kupata msaada wa kisheria mahakamani kadhalika kuisaidia serikali kutazama kwa upana na uhuru mahala ambapo haki za watu zinapokwa na baadhi ya makundi ya watu ama mamlaka, hatua itayoliweka taifa katika nafasi nzuri ya uzingatiaji wa haki za watu.