1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yaanza kuwapa raia umeme kwa mgao kufuatia ukame

24 Novemba 2022

Mamlaka za Tanzania zimeanzisha mgao wa umeme kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa umeme unaosababishwa na ukame ambao umeathiri vyanzo vya maji. Baadhi ya maeneo yatarajiwa kukosa huduma hiyo kwa saa tisa.

https://p.dw.com/p/4JzQc
Wie klimafreundlich ist die WM in Katar?
Picha: Anna Opoleva/PantherMedia/IMAGO

Akizungumza jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Maharage Chande amesema kampuni hiyo inakabiliwa na upungufu wa kati ya megawati 300 na 350.

Umeme bado ni mashaka makubwa tu Tanzania

Chande ametaja ukame wa muda mrefu na matengenezo yanayoendelea katika baadhi ya vituo vya kufuwa umeme kuwa sababu kuu mbili ambazo zinasababisha upungufu katika uzalishaji umeme.

Juhudi za Tanzania kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme

Tanzania inajaribu kuongeza uwezo wake wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji, ikiwa ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa mradi tata wa bwawa la Julius Nyerere katika Pori la Akiba la Selous, unaotarajiwa kuzalisha megawati 2,100 mara baada ya kuanza kutumika.

Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan alizindua mradi wa maji ikiwa ni pamoja na kuchimba visima katika mitaa ya jiji la Dar es Salaam. Wakaazi wa jiji hilo wamekuwa wakikumbwa na uhaba wa maji pia.
Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan alizindua mradi wa maji ikiwa ni pamoja na kuchimba visima katika mitaa ya jiji la Dar es Salaam. Wakaazi wa jiji hilo wamekuwa wakikumbwa na uhaba wa maji pia.Picha: President of Tanzania Office

Kumekuwa na wasiwasi  mkubwa nchini Tanzania kutokana na mgawo huo wa umeme unaoathiri maeneo mengi. Japo mamlaka nchini humo zinasema mgawo huo umesababishwa na hali ya ukame, wakosoaji wa mambo wanainyoshea kidole serikali kwa kushindwa kuweka vipaumbele vyake ili kuondokana na adha hiyo inayojitokeza mara kwa mara.

Licha ya ahadi za mara kwa mara za serikali kulitafutia ufumbuzi wa kudumu suala hilo, lakini linaonekana kuwa donda ndugu kwa vile linajitokeza kila mara na safari hii maumivu yake yanaonekana kugusa watu wa sekta zote.

Viwango vya maji vimepungua katika mabwawa

Kiasi cha umeme kinachoelezwa kupungua safari hii kinatajwa kufikia megawati 300 hadi 350 kwa siku na wakati akitoa tathmini ya hali ya mgawo huo, mkurugenzi mkuu wa shirika la umeme Tanzania(Tanesco) Maharage Chande amesema kiwango cha maji katika maeneo kama Kihansi, Bwawa la Mungu na maeneo mengine kipo chini mno.

Kwa maana hiyo hali ya mgawo huo huenda ukaandeelea kuathiri wengi hadi mwishoni mwa mwezi wa Disemba ingawa shirika hilo linasema limeweka mipango kadhaa kurejesha uzalishaji wa umeme.

Shughuli nyingi za kibiashara zinakwama kutokana na mgawo huo na makundi ya watu wanaofanya shughuli ndogondogo kama vile  vinyozi na wasusi wa salooni, biashara za viwanywaji baridi na shughuli nyingine za hapa na pale ndizo zinazoenelana kuumia zaidi.

Kilio cha wafanyabiashara

Lakini wafanyabiashara wakubwa na wenye kuendesha viwanda ambavyo uzalishaji wake hutegemea umeme kwa asilimia 100, hawajaachwa nyuma kwenye kilio hicho wakisikitika kwa namna wanavyoanguka kiuzalisha.

Wakosoaji wa mambo wanasema mamlaka zinazohusika na nishati zinapaswa kubeba mzigo wa lawama kwa kushindwa kuleta ufumbuzi wa kudumu kuhusu kadhia hii.

Mgawo wa umeme unakuja siku chache wakati makali ya mgawo wa maji ukianza kupungua katika baadhi ya maeneo huku mgawo huo ukiwa umeleta adhari kubwa.