1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

Tanzania yaanza kutekeleza amri ya kuvaa barakoa

George Njogopa20 Aprili 2020

Tanzania imeendelea kurekodi ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona ikikfikia watu 170, huku wakaazi wa jiji la Dar es Salaam wakianza kutekeleza agizo la kuvaa barakoa, na Marekani ikitangaza kuwaondoa raia wake.

https://p.dw.com/p/3bB9D
Tanzania Daressalam Fahrgäste mit Mundmasken
Picha: DW/S. Khamis

Ingawa wananchi wanaendelea na maisha ya kawaida lakini kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakichukua tahadhari na kuzingatia kanuni za afya. Hadi Jumapili Tanzania ilikuwa imerikodi visa 170 vya maambukizi ya virusi hivyo, huku Zanzibar pekee ikiwa na wagonjwa 53.

Dar es salaam inayokadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya milioni 5 ndiyo eneo pekee linaloandamwa zaidi na maambukizi hayo jambo lililowasukuma watendaji wa serikali kutangaza mikakati yenye lengo la kukabiliana na maambukizi hayo.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na utoaji wa elimu kwa wananchi kupitia matangazo ya umma, amri ya kuwataka watumiaji wote wa usafiri wa daladala kuvaa barakoa na sehemu ya uuzaji vyakula kuweka utaratibu maalumu wa utoaji wa huduma hiyo.

Uvaaji huo wa barakoa umetangazwa kuanza rasmi siku ya Jumatatu lakini kwa kiasi kikubwa kunashuhudiwa mkanganyiko wa mambo kwani baadhi wamekuwa wakivaa vitambaa jambo ambalo linadaiwa kuwa tofauti na maelekezo ya wataalamu wa afya.

Tansania Ummy Mwalimu
Waziri wa afya wa Tanzania Ummy MwalimuPicha: picture-alliance/Photoshot

Marekani kuondoa raia wake Tanzania

Katika hatua nyingine Marekani imeanza kuwaondosha raia wake walioko nchini kutokana na hofu hiyo ya virusi vya corona. Ubalozi wake nchini umewataka raia hao kujiandikisha tayari kwa kurejea makwao. Marekani inakuwa taifa la kwanza kuwatahadharisha raia wake na janga hilo na kuchukua hatua ya kuwarejesha nyumbani.

Afisa habari wa ubalozi wa Marekani jiji Dar es Salaam Benjamin Ellis, alisema hiyo ni sehemu ya juhudi za kihistoria za Marekani kuwaondoa raia wake kutoka maeneo yote duniani, yakiwemo maeneo ya mbali na vituo vilivyo na masharti makali ya karantini na vizuwizi vya usafiri.

"Wizara ya mambo ya nje haina kipaumbele kikubwa zaidi kuliko usalama wa raia wa Marekani walioko ng'ambo. Tunataka kukabiliana na changamoto hii iliyotokana na janga la covid-19, kila siku duniani kote," alisema Ellis 

Ama, kwa upande mwingine, ikiwa katika mkondo huo huo wa kujaribu kudhibiti maambukizi hayo, wizara ya ujenzi na uchukuzi imeanza utaratibu wa kukatisha tiketi ya usaifiri wa mabasi kwa kutumia mfumo mpya wa kieletroniki.

Chanzo: DW