1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yaahidi kuifanyia kazi sheria ya uchaguzi

Florence Majani4 Januari 2024

Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania, Dotto Bitteko amesema serikali itayafanyia kazi maoni yaliyotolewa na wadau kwenye mkutano maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa.

https://p.dw.com/p/4araY
Dotto Biteko Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania
Dotto Biteko Naibu Waziri Mkuu wa TanzaniaPicha: Ericky Boniphace/DW

Akihitimisha mkutano huo Alhamisi jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Mkuu, Doto Bitteko, amesema sheria zinazoboreshwa ni kwa ajili ya kulijenga taifa lenye maridhiano na hivyo serikali itayabeba maoni hayo na kuyafanyia kazi.

Bitteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati, amesisitiza kuwa majadiliano hayo ni mwanzo wa kujenga maridhiano ya kitaifa na kuwa sheria hizi zinarekebishwa kwa ajili ya Watanzania.

Msimamo huo umetolewa pia na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, ambaye amewaondoa hofu wadau kuwa maoni yao hayatachakachuliwa bali yatachukuliwa yote, tena kwa kuandikwa.

Mkutano huu Maalum wa baraza la vyama vya siasa umewakusanya wadau wa demokrasia kutoka vyama vya siasa, asasi za kiraia, viongozi wa dini, wa kimila, wawakilishi wa makundi maalum na asasi za kimataifa.

Mageuzi ya Tume ya Uchaguzi

Mkutano maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa uliojadili miswada ya sheria za uchaguzi, sheria ya vyama vya siasa na sheria ya Tume ya Uchaguzi
Mkutano maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa uliojadili miswada ya sheria za uchaguzi, sheria ya vyama vya siasa na sheria ya Tume ya UchaguziPicha: Florence Majani/DW

Awali, wadau hao walipata fursa ya kutoa maoni yao wakipigilia msumari maboresho ya Tume ya Uchaguzi, wakishauri watendaji wa tume kuanzia ngazi ya juu hadi ya chini wasitokane na serikali wala wasichaguliwe na rais. Wakashauri matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano wakati wa uchaguzi na ushiriki wa wanawake katika uongozi.

Kuhusu matumizi ya Tehama wakati wa uchaguzi, mchambuzi wa masuala ya kisiasa Deus Kibamba alishauri michakato yote ya uchaguzi itumie Tehama ili kuhakikisha vijana wengi wanashiriki uchaguzi kwa njia ya mtandao.

Suala la ushiriki wa wanawake katika uchaguzi na uongozi liliibuliwa na wadau walio wengi, wakitaka miswada hiyo iweke bayana kipaumbele kwa wanawake, huku wadau wakiibua suala la rushwa ya ngono na mgombea huru asiye na chama.

''Toa Maoni yako kuimarisha demokrasia''

Toa Maoni Yako Kuimarisha Demokrasia kauli mbiu ya mkutano wa Dar es Salaam
Toa Maoni Yako Kuimarisha Demokrasia kauli mbiu ya mkutano wa Dar es SalaamPicha: Florence Majani/DW

Wadau katika mkutano huo ulioanza jana Jumatano,  wameelezwa kuwa chimbuko la mkutano huo ni R nne za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambazo zinajikita katika mabadiliko, uvumilivu, maridhiano na ujenzi.

Mkutano huo uliobebwa na kaulimbiu isemayo, Toa Maoni Yako Kuimarisha Demokrasia umehitimishwa leo huku wadau wakihimizwa kuendelea kutoa maoni yao ili kuboresha miswada hiyo. Florence Majani. DW. Dar es Salaam.