1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Wito watolewa wa kukomesha unyanyasaji wa kingono

Hawa Bihoga25 Novemba 2020

Watetezi wa haki za wanawake watoa wito wa kuanzishwa kwa madawati ya jinsia katika vyuo vikuu na taasisi za elimu nchini Tanzania, kwa lengo la kukabiliana na tatizo la unyanyasaji wa kingono unaotajwa kukithiri.

https://p.dw.com/p/3lnT8
Tansania Corona l Studenten in einer Vorlesung in Nairobi
Picha: Xinhua/Imago Images

Wito huo umetolewa kuelekea kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, inayoanza Jumatano ambapo Ulimwengu unaadhimisha Siku ya Kupambana na Unyanyasaji dhidi ya Wanawake.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya kuzuwia na kupambana na rushwa nchini TAKUKURU, ukivihusisha vyuo vikuu vya Dar es Salaam na Dodoma, asilimia 50 ya waliohojiwa walieleza uwepo wa rushwa ya ngono katika vyuo vikuu, huku asilimia 29.9 ya wafanyakazi wakieleza kuwepo kwa ushawishi wa makusudi ili kujipatia huduma kutoka kwa mamlaka.

Sababu tano ambazo ni ukosefu wa maadili, ushawishi wa mtu mwenye mamlaka, mfumo wa utoaji taarifa kutokuwa rafiki, mifumo dhaifu ya kushughulikia rushwa ya ngono na mamlaka ya kutoa alama za mtihani kuachwa chini ya walimu pekee ndio zimetajwa kuwa vyanzo vikuu vya rushwa ya ngono, huku ukosefu wa maadili ukichangia tatizo hilo kwa karibu asilimia 70.

Vijana wakosa majukwaa ya kuzungumzia adha za rushwa ya ngono

Daktari Katanta Simwanza, Mshauri Mwandamizi wa afya ya Jamii na Jinsia anasema kundi la watu walioko vyuoni hawana pa kuzungumzia adha za rushwa ya ngono zinazowakabili, na hivyo kuna haja ya kuunda madawati ya jinsia vyuoni ili kuwapa jukwaa la kuelezea masaibu yao.

Mbali na majukwa hayo kuzungumzia ukatili wa kingono, yatatumika pia kuzungumzia ukatili wa kijinsia ambao wanafunzi na watumishi vyuoni wamekuwa wakikumbana navyo majumbani na nje ya nyumbani, kama vile ukeketaji, kubakwa pamoja na mimba za utotoni. 

Kampeni ya siku 16 ya kupambana na ukatili wa kijinsia, inanuwia kuihamasisha jamii juu ya tatizo la ukatili wa kijinsia na rushwa ya ngono.
Kampeni ya siku 16 ya kupambana na ukatili wa kijinsia, inanuwia kuihamasisha jamii juu ya tatizo la ukatili wa kijinsia na rushwa ya ngono.Picha: DW/N. Quarmyne

Sheria ya kupambana na kuzuwia rushwa nchini Tanzania imeweka kifungu makhsusi cha kuzuwia rushwa ya ngono ambacho kinabainisha kuwa ni kosa kwa mtu mwenye mamlaka kudai au kuomba rushwa ya ngono kwa mtu yeyote kama sharti la kutoa ajira, upendeleo, kumpandisha cheo, kumpatia haki au huduma maalum.

Katika maboresho yaliofanywa na serikali kuhusu sheria hiyo, kosa la rushwa ya ngono limetajwa kuwa moja ya makosa 7 ya uhujumu uchumi, na adhabu yake kwa mtu anaekutwa na hatia ni kifungo kisichopungua miaka 20 na kisichozidi miaka 30. Je, mkakati huu utaleta tija kwa waathirika wa tatizo hili. 

Kampeni ya siku 16 ya kupambana na ukatili wa kijinsia, inanuwia kuihamasisha jamii juu ya tatizo la ukatili wa kijinsia na rushwa ya ngono ambayo yametajwa kuathiri vizazi vya sasa na vijavyo, huku kaulimbiu ya kampeni ya mwaka huu ikiwa inasema: Kupinga Ukatili wa Kijinsia, Inaanza na Mimi. Hawa Bihoga, DW, Dar es Salaam.