1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Rais Samia Suluhu aendelea na ziara yake Mwanza

14 Juni 2021

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan yuko ziarani mkoani Mwanza akikagua miradi ya maendeleo. Katika ziara hiyo Rais Samia amezindua rasmi ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga

https://p.dw.com/p/3utOQ
Samia Suluhu, Vizepräsidentin Tansania
Picha: DW/Said Khamis

Uzinduzi wa ujenzi wa kipande hicho cha reli ni ishara ya kuanza kwa ujenzi wa kipande hicho cha tano kinachojengwa ndani ya miezi 36 sawa na miaka mitatu. Kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo ya kisasa nchini Tanzania kutasaidia kutatua kero ya usafiri kwa kusafirisha mizigo na abiria kwa uharaka zaidi katika nchi za ukanda wa maziwa makuu.

Rais Samia  amezindua kipande hicho cha reli kutoka Mwanza hadi Shinyanga chenye urefu wa kilometa 341, ambapo kilometa 219 zitatumika kama njia kuu huku kilomita 122 zitatumika kama njia za kupishana  na vituo vya kushuka na kupanda abiria ni 9, huku idadi ya vivuko vya chini  vitakavyojengwa ni 44 na vya juu vitakuwa ni 23.

Mapema mwezi Januari mwaka huu, serikali za Tanzania na china zilitiliana saini za makubaliano ya ujenzi wa reli ya kisasa ambao utagharimu jumla ya shilingi za kitanzania  trilioni 3.1 sawa na zaidi ya dola za kimarekani bilioni 1.326.

Kuanza kwa ujenzi wa reli hiyo ya kisasa nchini Tanzania, kunatajwa kuwa na tija hasa kwa wananchi wa mikoa hiyo kwani zaidi ya ajira elfu 75 zinatajariwa kupatikana kwa miaka yote mitatu ya ujenzi wa reli hiyo.

Kuwekwa kwa jiwe la msingi ni kiashiria cha kuanza kujengwa kwa kipande cha tano, ambapo kipande cha kwanza ni kutoka dar es salaam hadi Morogoro, Morogoro hadi Makutupora, Makutopora kwenda Tabora, Tabora mpaka Isaka na Isaka hadi jijini Mwanza.

Wananchi wana matarajio makubwa

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa mkoa wa Mwanza mbali na kuona miradi hii inakwenda kubadili mandhari ya jiji la Mwanza ,wanaona miradi hii itabadili uchumi wa ukanda huo unaounganisha mataifa ya Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.

Rais Samia yupo jijini Mwanza kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambapo amefanikiwa kufungua miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kiwanda chenye mtambo wa kusafishia dhahabu kilichopo eneo la Sabasaba wilayani Ilemela, jengo jipya la benki kuu Tanzania kanda ya ziwa (BOT) na ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa daraja la Magufuli lilolopo Kigongo Busisi lenye urefu wa kilometa 3.2 na upana wa mita 28.45 linalojengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 60 sawa na zaidi ya dola  milioni 26.086 za kimarekani

Kesho Rais huyo wa kwanza mwanamke Tanzania atahitimisha ziara yake kwa kuongea na vijana wa Tanzania kupitia vijana wa mkoa wa Mwanza katika Uwanja wa Michezo wa Nyamagana