1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfghanistan

Taliban yakatiza mahusiano na baadhi ya balozi zake

30 Julai 2024

Serikali ya Taliban nchini Afghanistan imekatiza mahusiano na balozi zake zilizoko katika mataifa ya Magharibi na kusema haitatambua hati za usafiri wala vibali vya kusafiri vitakavyotolewa na balozi hizo.

https://p.dw.com/p/4ivGA
Waziri wa mambo ya nje wa serikali ya Taliban nchini  Afghanistan Amir Khan Mutaqqi( kushoto) ahudhuria mkutano wa 5 wa mashauriano ya Moscow kuhusu Afghanistan katika Ukumbi jijini Kazan mnamo Septemba 29, 2023.
Viongozi wa serikali ya Taliban nchini AfghanistanPicha: Yegor Aleyev/TASS/IMAGO

Hatua hii ya Taliban ni jaribio la hivi karibuni zaidi la kudhibiti balozi za Afghanistan zilizoko katika nchi za magharibi, tangu kundi hilo liliporejea madarakani  mnamo mwaka 2021. Viongozi wengi wa serikali ya Taliban wamewekewa vikwazo na hakuna taifa linalowatambua kama watawala halali wa Afghanistan.

Soma pia;Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Afghanistan wafunguliwa Doha

Lakini katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, utawala huo,ulioingia madarakani baada ya vikosi vya magharibi kuondokaAfghanistan, umewaweka mabalozi kutoka kundi lake katika baadhi ya balozi za mataifa jirani kwenye kanda hiyo.

Serikali ya Taliban kutokubali paspoti na nyaraka nyingine za balozi ilizozitupia mkono

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X, Zia Ahmad Takal, naibu msemaji wa wizara ya mambo ya nje inayoendeshwa naTalibanamesema kuwa kufuatia notisi hiyo, huduma kama vile hati, kutoa pasipoti, viza na nyaraka nyingine muhimu katika balozi za nchi yao huko London, Ubelgiji, Berlin, Bonn, Uswisi, Austria, Ufaransa, Italia, Ugiriki, Poland, Norway, Canada na Australia, hazikubaliwi tena na wizara ya mambo ya nje, na kwamba  wizara hiyo haina jukumu lolote tena juu ya hati hizo na hakuna hatua itakayochukuliwa kuzihusu.

Raia wa Afghanistan kutafuta huduma kwa balozi nyingine mbali na zilizoorodheshwa

Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa raia wote wa Afghanistan wanaoishi nje ya nchi pamoja na wageni wanaweza kutembelea balozi za nchi hiyo zilizoko katika nchi nyingine mbali na zilizoorodheshwa ili kupata huduma za kibalozi.

Wasichana wahudhuria shule siku ya kwanza ya kufunguliwa shule mnamo Machi 25, 2023 mjini Kabul nchini Afghanistan
Wasichana wahudhuria shule mjini Kabul nchini AfghanistanPicha: Ebrahim Noroozi/AP Photo/picture alliane

Pakistan, China na Urusi,  ni miongoni mwa balozi za Afghanistan zinazofanya kazi kwa maagizo ya serikali ya Taliban.

Balozi zilizowekewa vizuizi zakabiliwa na hali mbaya ya kifedha 

Balozi hizo zilizowekewa vizuizi na serikali ya mjini Kabul zimejikuta katika hali mbaya ya kifedha, zikitegemea sana ada za ubalozi kulipa mishahara ya wafanyikazi, kodi za majengo na gharama nyingine.

Bila mapato hayo huenda zikakabiliwa na wakati mgumu kuendelea kuhudumu.

Hata hivyo, wizara ya mambo ya nje haikujibu ombi la tamko kuhusu mipango yake ya baadaye kuhusu balozi hizo.

Taliban yang'ang'ana kuwa mwakilishi wa pekee wa Afghanistan kimataifa

Tangu Taliban iliporejea madarakani kwa kutumia nguvu baada ya uasi wa miongo miwili, maafisa wake wamekuwa waking'ang'ana kuwa wawakilishi wa pekee wa Afghanistan katika jukwaa la kimataifa.

Serikali ya Taliban yanyimwa nafasi ya ubalozi katika Umoja wa Mataifa

Watawala hao waliotengwa kutokana na vitendo vyao dhidi ya wanawake, wamenyimwa nafasi ya ubalozi katika Umoja wa Mataifa. Kiti cha nchi hiyo katika Umoja huo wa Mataifa bado kinashikiliwa na serikali ya zamani iliyokuwa ikiongozwa na Ashraf Ghani.

Soma pia:Taliban washiriki mkutano wa faragha na Umoja wa Mataifa Doha

Hata hivyo katika mazungumzo yaliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa mjini Doha,nchini Qatar mwezi uliopita, waliiwakilisha Afghanistan huku makundi ya asasi za kiraia wakiwemo wanaharakati wa wanawake wakikosa kujumuishwa katika mazungumzo makuu.

Wachambuzi, wanaharakati wa haki na wanadiplomasia wamegawanyika kuhusu iwapo watashirikiana na serikali ya Taliban katika jitihada za kulegeza msimamo wao au kuwatenga hadi warudi nyuma.