1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Taliban yaadhimisha miaka miwili tangu kurejea madarakani

15 Agosti 2023

Utawala wa Taliban nchini Afghanistan unaadhimisha miaka miwili leo tangu ulipochukua madaraka na kulirejesha taifa hilo chini ya sheria kali za kidini zinasokoselewa na Jumuiya ya Kimataifa

https://p.dw.com/p/4VBGJ
Afghanistan Kabul | Sticker mit Taliba Führer Hibatullah Achundsada
Picha: Mohd Rasfan/AFP/Getty Images

Bendera za Emirati ya Kiislamu ya Afghanistan - jina ambalo watawala wa Taliban wameipatia nchi hiyo - zimeonekana zikipepea katika vituo vya upekuzi kwenye mji mkuu, Kabul, kuadhimisha siku ambayo serikali iliyokuwa ikiungwa mkono na mataifa ya magharibi ilianguka na Taliban wakachukua madaraka.

Soma pia: Kiongozi wa juu Afghanistan aonya dhidi ya mashambulizi nje ya nchi

Taarifa iliyotolewa na mamlaka za nchi hiyo imeitija Agosti 15 mwaka 2021 kuwa siku ya ushindi iliyofungua njia ya kuundwa kwa "utawala wa Kiislamu nchini Afghanistan."

Kupitia taarifa hiyo Taliban wamesema kukamatwa kwa mji Kabul miaka miwili iliyopita kulidhihirisha kwa mara nyingine kwamba hakuna nguvu kutoka nje inayoweza kuitawala Afghanistan.

Tangu kuingia madarakani serikali ya Taliban imepitisha sheria kali za Kiislamu hususani zinazoweka vizuizi kwa wanawake na ambavyo Umoja wa Mataifa umevitaja kuwa "ubaguzi wa kijinsia."