1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban watoa amri ya kuheshimu haki za wanawake

Sylvia Mwehozi
3 Desemba 2021

Utawala wa kundi la Taliban umetoa amri mpya kupitia jina la kiongozi mkuu wa Afghanistan likiziamuru wizara zote nchini humo kuchukulia kwa uzito mkubwa haki za wanawake.

https://p.dw.com/p/43nZ9
Afghanistan | World Food Program in Kabul
Picha: Bram Janssen/AP Photo/picture alliance

Hatua hiyo inakuja baada ya Taliban kudhibiti mamlaka katikati ya mwezi Agosti na kujaribu kuzifikia mali za mabilioni ya dola na misaada iliyositishwa wakati wa utawala uliopita uliokuwa ukiungwa mkono na mataifa ya magharibi.

"Uongozi wa Emireti ya Kiislamu unatoa maelekezo kwa taasisi zote....kuchukua kwa uzito hatua za kutekeleza haki za wanawake", ilisema amri hiyo ikimnukuu kiongozi wa juu Hibatullah Akhundzada.

Amri hiyo imetuama katika haki za ndoa na wajane, ikisema kwamba "hakuna mtu anayepaswa kumlazimisha mwanamke kuolewa kwa lazima au shinikizo" na kwamba mjane anayo haki ya kupata sehemu isiyotajwa ya urithi wa mumewe.

Pia imetamka wazi kwamba kuanzia sasa mjane ataruhusiwa kuolewa tena wiki 17 baada ya kufiwa na mumewe na atakuwa na uhuru wa kujichagulia mume. Kwa kawaida mjane aliruhusiwa kuolewa na kaka au ndugu ya mumewe baada ya kifo.

Afghanistan Emir der Taliban Mawlawi Hibatullah Akhundzada
Kiongozi mkuu wa Afghanistan Hibatullah AkhundzadaPicha: CPA Media Co. Ltd/picture alliance

Aidha, amri hiyo imeielekeza wizara ya utamaduni na mawasiliano kuchapisha taarifa juu ya haki za wanawake ili kukomesha ukandamizaji unaoendelea. Wanawake nchini Afghanistan kwa miongo kadhaa wamechukuliwa kama mali, wakati fulani hutumika kama fidia kwa familia ya mtu aliyeuwawa, au kumaliza migogoro na uhasama wa kikabila. Lakini sasa utawala wa Taliban umepiga marufuku desturi hiyo.

Hata hivyo amri hiyo haikutaja sehemu yoyote juu ya elimu ya sekondari kwa wasichana, ambayo kufikia sasa imesitishwa kwa mamilioni ya wanafunzi wa kike au pia ajira za wanawake ambao walizuiwa kurejea maofisini hasa katika sekta ya umma.

Haki za wanawake zilikuwa zimebanwa vikali wakati wa utawala uliopita wa Taliban kuanzia mwaka 1996 hadi mwishoni mwa 2001. Wafadhili muhimu wa kimataifa wamekuwa wakitaka Afghanistan kuheshimu haki za wanawake kama sharti la kurejeshwa kwa misaada nchini humo.

Wanawake hulazimika kuvaa mavazi ya kujifunika mwili mzima, kuruhusiwa kutoka nyumbani tu wakisindikzwa na mwanaume na kupigwa marufuku ya kazi na elimu.

Kiongozi mkuu Akhundzada hajaonekana hadharani tangu achukue wadhifa huo mwaka 2016, baada ya mtangulizi wake kuuwawa katika shambulio la Marekani la ndege zisizokuwa na rubani.

Mwishoni mwa Oktoba Taliban walitoa mkanda wa sauti wa dakika 10 wa kiongozi huyo alipokuwa akihutubia Madrassa katika mji wa kusini wa Kandahar. Lakini baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa kiongozi huyo huenda ameuawa mwaka mmoja au zaidi iliyopita.

Vyanzo : reuters/ap