1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban lasema litajibu kwa mashambulizi

Ibrahim Swaibu
13 Mei 2020

Katika taarifa yake Jumanne kundi hilo la wanamgambo limesema litaendelea na mashambulizi dhidi ya vikosi vya Afghanistan iwapo litalengwa katika operesheni ya vikosi vya serikali.

https://p.dw.com/p/3cAuk
Afghanistan Taliban im Gefängnis
Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Gul

Taliban limeonya kuwa litajibu kwa mashambulizi iwapo serikali ya Afghanistan itaanza tena kufanya operesheni dhidi yake. Hii ni kufuatia mashambulizi ya Jumanne ambayo serikali imesisitiza kuwa yaliketekelezwa na kundi hilo huku rais  Ashraf Ghani akisema  vikosi vya Afghanistan vitaanza tena kuchukua hatua dhidi ya Taliban na makundi mengine ya Kigaidi.

Ghani  amelishtumu kundi hilo kwa kutekeleza mashambulizi ya Jumanne dhidi ya hospitali ya kina mama wajawazito katika mji mkuu Kabul liliosababisha  vifo vya watu  24 wakiwemo watoto wadogo na wauguzi. Kadhalika siku hiyo hiyo watu wapatao 25 waliokuwa wakihudhuria mazishi waliuawa katika shambulio mashariki mwa nchi hiyo.

Kundi linalojiita dola la Kiislamu IS limedai kutekeleza shambulio dhidi ya waombolezaji lakini hadi sasa hakuna kundi limedai kuhusika na shambulio dhidi ya hosiptali. Wizara ya afya nchini humo imesema leo kuwa idadi ya waliofariki katika shambulio la hospitali sasa imefikia watu 24 na majeruhi 16.

Msemaji wa serikali ya Afghanistan Sediq Sediqqi amesema serikali kamwe haitokubali kwamba  mashambulizi ya jana hayakutekelezwa na Taliban. Hatahivyo Taliban wamekanusha kuhusika katika mashambulizi hayo.

Rais Ghani alisema vikosi vitachukua tu hatua za kujilinda bila kuwashambulia Taliban kama moja ya ahadi ya upande wa serikali yake kuheshimu makubaliano kati ya kundi hilo na Marekani huku serikali yake pia ikitarajia kuanza majadiliano ya moja kwa moja na Taliban.

Katar Doha Unterzeichnung Abkommen USA Afghanistan  Taliban Zalmay Khalilzad Abdul Ghani Baradar
Mjumbe maalum wa Marekani nchini Afghanistan Zalmay Khalilzad (kushoto) na mkuu wa kisiasa wa kundi la Taliban Mullah Abdul Ghani Baradar wakisaini makubaliano mjini Doha Qatar.Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Sayed

Tangu kufikia makubaliano kati ya Marekani na Taliban mnamo Februari, Taliban imejiepusha kwa sehemu kubwa kufanya mashambulizi dhidi ya Kabul. Moja ya vipengee vya makubaliano  kati ya Taliban na Marekani  ni vikosi vyote vya Marekani na vya kigeni kuondoka kutoka ardhi ya Afghanistan katika mwaka ujao.

Hatahivyo, kutokana na hali tete iliopo kwa sasa, kuna khofu ya kuvurugika kwa mchakato wa amani kusuluhisha mgogoro kati ya Taliban na serikali ya nchi hiyo.

Katika taarifa yake mara baada ya mashambulizi hayo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo alitoa wito kwa  Taliban na serikali ya Afghanistan kushirikiana kuhakikishia kuwa kuna utendaji wa haki na kuwaadhibu wahusika wa mahambulizi

Mjumbe maalumu wa Marekani nchini Afghanistan Zalmay Khalizad amezitaka Taliban na serrikali ya Afghanistan kushirikiana katika kuleta amani nchini humo.

Vyanzo: AFPE/ DPAE/RTRE