SUVA : Jumuiya ya kimataifa yalani mapinduzi Fiji
6 Desemba 2006Ikiwa ni siku moja baada ya mapinduzi ya kijeshi katika kisiwa cha Bahari ya Pasifiki cha Fiji jumuiya ya kimataifa imekuwa na sauti moja katika kulaani mapinduzi hayo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan amelitaka jeshi kuirudisha madarakani serikali iliochaguliwa kidemokrasia. Marekani imesitisha msaada wa dola milioni 2.5 kwa nchi hiyo wakati Uingereza imesimamisha msaada wa kijeshi kwa kisiwa hicho.
Katika mapinduzi ya nne kufanyika kisiwani Fiji Mkuu wa majeshi Frank Bainimarama amempinduwa Waziri Mkuu Laisenia Qarase hapo jana kwa kumshutumu kwa rushwa na kushindwa kuwafungulia mashtaka waliohusika na mapinduzi ya mwisho katika kisiwa hicho.
Mitaa ya mji mkuu wa Suva leo asubuhi ilikuwa shwari na Qarase amesafirsihwa kutoka mji mkuu na kupelekwa kwenye kisiwa alikozaliwa cha Vanua Balavu.