1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SURA YA UJERUMANI -UCHAGUZI WA BAVARIA

19 Septemba 2003
https://p.dw.com/p/CHeP

Sura ya Ujerumani leo inawasimulia juu ya uchaguzi wa jumapili hii wa mkoa wa Bavaria-wenye mji mkuu wake Munich,makao ya serikali ya mkoa huo.
Wapiga kura milioni 9 wanatia kura jumapili hii kuamua sura ya Bunge hilo na hakuna anaetia shaka kuwa chama-tawala cha Christian Social Union,kinachoongozwa na Bw.Edmund Stoiber,waziri-mkuu wa Bavaria na mtetezi-mkuu wa wadhifa wa ukanzela kati yake na Kanzela Schröder katika uchaguzi uliopita-kitarudi madarakani. Swali CSU kitashinda kwa wingi mkubwa gani mbele ya chama kikuu cha Upinzani cha SPD cha Kanzela Gerhard Schröder.

Itakua msisimko mkubwa ikiwa jumapili hii, waziri-mkuu Edmund Stoiber,anaetawala Bavbaria tangu miaka 10 sasa akiangushwa madarakani.Kinyume chake: uchunguzi wote wa maoni unaonesha chama chake-tawala CSU kitajipatia tena wingi mkubwa.Chama cha CSU kinachotawala Bavaria mfululizo tangu miaka 4o sasa ni chama ndugu na kile cha taifa cha Christian Democratic party-CDU.CSU kinajitapa mno kwa ustadi wake wa uongozi mkoani bavaria lakini pia kutetea uhuru wa jimbo la Bavaria katika siasa za shirikisho la Ujerumani.

Katika Bunge la shirikisho la Bundestag- mjini Berlin,chama cha CSU huunda kundi moja la wabunge na chama hicho kikuu cha upinzani cha CDU na hii tangu kuundwa kwa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani miaka 54 iliopita.Katika kila uchaguzi wa Bunge la Shirikisho vyama hivi-ndugu -CDU na CSU huchangia pamoja watetezi wao na hawapingani.
1980,Franz-Josef Strauss aliekua kiongozi maarufu wa chama hicho na waziri-mkuu wa Bavaria kwa miaka mingi aligombea wadhifa wa ukanzela wa Ujerumani lakini alishindwa na kanzela Helmut Schmidt kutotoka chama cha Kanzela wa sasa Gerhárd Schröder. Na katika uchaguzi uliopita mwaka 2000,alishindwa waziri-mkuu wa sasa wa Bavaria Edmund Stoiber kwa kura chache tu na Gerhard Schröder. Kwahivyo, uchaguzi wa jumapili hii kwa jicho la chama cha CSU na mwenyekiti wake Stoiber ni kulipioza kisasa kwa chama cha bw.Schröder na yeye mwenyewe. Stoiber anauliza:

"Tizama ahadi gani zilizotolewa ? mwaka baada ya uchaguzi mkuu wa shirikisho,hakuna kilichotengenea bali kila kitu kimezidi kuharibika.Mambo kabisa hayawezi kuendelea namna hivi.Mwaka huu hakuna hata mageuzi yoyote yaliopitishwa na kugeuka sheria."-alalamika Bw.Stoiber-waziri-mkuu wa Bavaria.

Dhidi ya Bw.Stoiber , chama cha Social Democrat hakina jibu,kwani ni koboko yao alao katika mkoa wa Bavaria. Kwa muujibu wa uchunguzi wa maoni, chama cha SPD kinaelekea kujipatia matokeo yake mabaya kabisa katika historia ya uchaguzi mkoani Bavaria-yaani 20% tu ya kura. Matatizo 2 makubwa yanakikabili chama cha upinzani mkoani Bavaria-SPD: Tatizo la kwanza : kutokana na mabishano juu ya mradi wa sera za mageuzi za serikali ya muungano wa chama cha SPD na Kijani na kutokana pia na hali ya msukosuko wa uchumi isiopatiwa bado ufumbuzi, SPD mkoani bavaria hakipati upepo mzuri wa kukipeperusha juu kutoka serikali kuu ya Berlin.
Pili:Mtetezi mkuu katika uchaguzi huu anaekiwakilisha chama hiki cha SPD, Franz Maget hajulikani sana mkoani Bavaria.Hata kufanyiwa kwake ujasusi na kutishwa na wafuasi wa kinazi-mambo-leo hakujabadili kitu-mkasa ambao umefichuliwa muda mfupi kabla ya uchaguzi huu.

Kwahivyo chama cha SPD na mtetezi wake mkuu Maget kimeishia kutoa mwito kuwataka wapigakura wa mkoa huu wasikipe chama-tawala cha CSU wingi mwengine wa thuluthi-mbili Bungeni-jambo ambalo zitaupunguzia nguvu za upinzani kuikosoa serikali.Bw.Mageti anasema:

"Haitawezekana tena kumshtaki waziri yeyote,wenyekiti wa halmashauri mbali mbali waweza kuondoshwa kwa wingi wa kura za thuluthi-mbili wakionekana wanaleta kero kwa serikali.Haitawezekana hata kuitisha kikao maalumu cha Bunge hilo la mkoa tukikabiliwa na wingi wa thuluthi-mbili."

Jumla ya wapigakura milioni 9 wanakwenda kupiga kura.Katika bunge la bavaria kenye jengo la Maximilianeum huko Munich,wanaingia wabunge 180-hii ni wabunge 24 kasoro kuliko ilivyokua katika uchaguzi uliopita miaka 5 nyuma. Mbali na chama cha CSU na SPD,wabunge wa chama cha Kijani cha walinzi wa mazingira wanatarajiwa kuchaguliwa tena .Chama kidogo cha kiliberali cha FDP kinaweka matumaini pia ya kurudi katika bunge hili baada ya kupita miaka 13.Chama hiki kinachjoongozwa na waziri wa sheria wa zamani Bibi Sabine Leutheusser-Schnarrenberger,kimeangukia kima cha 4% ya kura katika uchunguzi wa maoni.Na hivyo kiko chini kidogo ya mpaka wa 5% unaohitajika ili chama kuwakilishwa Bungeni.

Mkoa wa Bavaria unajivunia jiji lake kuu la Munich.Lakini, si Wabavaria tu waishio katika mkoa huu.Upande wa kaskazini mwake wakaazi wanasisitiza asili yao ya Franken.Upande wa mashariki mtu hujinasibu kwanza ni Oberpfälzer na magharibi kandoni mwa mji wa Augsburg wanaishi Waschwabe.Ni wilaya 2 tu kati ya 7 za utawala-yaani mji mkuu Munich na Niederbayern kandoni mwa Landshut ndio shina hasa la wabavaria.

Mbali na uchaguzi wa Bunge la mkoa ,jumapili hii inaamuliwa na wapiga kura halkadhalika, serikali mbali mbali za mitaa.Isitoshe kuna kura 2 za maoni zinazohusika na kubadili katiba.Moja inahusu serikali ya mkoa kukabidhi majukumu yale tu ambayo fedha za kuyagharimia zimehakikishwa kuwapo.Mageuzi mengine ni kuruhusu umri wa kupiga kura kwa bunge la mkoa uteremshwe na kuwa miaka 18 na haki za watoto kuimarishwa.

Uchumi wa bavaria umekua ukikua na kuimarika na waziri wa uchumi wa mkoa huo Otto Wiesheu anadai kuwa, mnamo miaka 10 iliopita uchumi umepanda marudufu.Bidhaa zinazosafirishwa n'gambo zimeongezeka kutoka kima cha 30% na kufikia 48%.na hizo anadai ni tarakimu za kujivunia mno ambazo mikoa mingine ya Ujerumani haiwezi kujitapa kuzifikia.
Nae waziri-mkuu Edmund Stoiber,akilenga mizinga yake kwa serikali kuu ya Berlin na kwa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, anasema:

"sisi ndio mkoa pekee nchini Ujerumani ambao nakisi ya ya bajeti yetu haikuvuka kile kima cha 3%.na mwakani ujerumani kipigwa faini kwa kukiuka sharti hilo lililowekwa na mkataba wa Maastricht,basdi nimeshabainisha wazi kuwa mkoa wa bavaria hautachangia kulipa faini hiyo."-asema waziri-mkuu wa bavaria Edmond Stoiber.
Macho basi ya wajerumani na vyama vya kisiasa mwishoni mwa wiki hii yanakodolewa mkoani Bavaria ambako hakuna shaka juu ya ushindi wa chama-tawala cha CSU.