1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yawahukumu kifo wanajeshi 27 kwa kumuua mwandamaji

30 Desemba 2019

Mahakama moja ya Sudan imewahukumu adhabu ya kifo maafisa 27 wa vikosi vya usalama kwa kumtesa na kumuua mwandamanaji mmoja wakati wa maandamano ya kumpinga aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir

https://p.dw.com/p/3VUuy
Sudan | Proteste um den Tod des Lehrers Ahmed Al-Khair
Picha: AFP/A. Shazly

Kifo cha mwandamanaji Ahmed al-Khair, aliyekuwa mwalimu wa shule, wakati alipokuwa kizuizini mwezi Februari kilikuwa suala muhimu na ishara katika maandamano hayo ambayo hatimaye yalisababisha jeshi kumuondoa al-Bashir madarakani.

Hukumu za leo, ambazo zinaweza kukatiwa rufaa, ndizo za kwanza kuhusiana na mauaji ya waandamanaji katika mapinduzi hayo.

Hukumu ya leo katika kesi dhidi ya vikosi vya usalama ilitolewa katika mahakama ya Omdurman, mji ndugu wa Khartoum, ambako waandamanaji kadhaa walikusanyika nje ya mahakama, wakidai haki kwa ajili ya al-Khair.

Al-Khair alikamatwa Januari 31 katika mkoa wa mashariki wa Kassala na akaripotiwa kufariki siku mbili baadaye. Mwili wake ilipelekwa kwenye hospitali ya eneo hilo ambako familia yake ilisema ulikuwa na michubuko. Kwa wakati huo, polisi ilikanusha kufanya kosa lolote ikisema kifo chake kilitokana na ugonjwa, bila kutoa maelezo yoyote.

Sudan | Proteste um den Tod des Lehrers Ahmed Al-Khair
Waandamanaji Sudan walishangilia wakati hukumu ikitolewaPicha: AFP/E. Hamid

Mahakama hata hivyo imesema leo kuwa mwalimu huyo alipigwa na kuteswa wakati akiwa jela. Watu 27 waliohukumiwa ni polisi waliokuwa kwenye gerela ambalo al-Khair alizuiliwa au majasusi wa eneo hilo.

Pia mwezi huu, mahakama mjini Khartoum ilimkuta al-Bashir na hatia ya makossa ya utakatishaji fedha na rushwa, na kumhukumu kifungo cha miaka miwili kwenye gereza lenye ulinzi mdogo.

Amnesty International na makundi mengine ya haki za binaadamu yametoa wito kwa serikali mpya kuviwajibisha vikosi vya usalama kwa kuwauwa watu wakati vilipofanya juhudi za kuyavunja maandamano dhidi ya utawala wa kijeshi, na hasa wale waliohusika na ukandamizaji mbaya dhidi ya waandamanaji waliokuwa wamekita kambi nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum Juni mwaka jana.

Tangu Desemba mwaka jana, karibu waandamanaji 200 wameuawa nchini Sudan. Sudan iko chini ya shinikizo kubwa la kimataifa na kikanda kufanya mageuzi. Huku uchumi ukiwa ukingoni mwa kuporomoka, serikali mpya ya inafanya juhudi za kutaka Sudan iondolewe kwenye orodha ya mbaya ya Marekani ya mataifa yanayofadhili ugaidi ili iweze kupokea msaada wa kigeni unaohitajika kwa kiasi kikubwa.