1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yautaka Umoja wa Mataifa kuthibitisha wakimbizi wamerejea makwao kwa hiari.

Josephat Charo29 Septemba 2004

Serikali ya Sudan imeutaka umoja wa mataifa kuthibitisha kwamba wakimbizi elfu 190 kutoka eneo lililokumbwa na machafuko la Darfur, wamerudi nyumbani kwao kwa hiari.

https://p.dw.com/p/CHiR
Kiongozi wa shirika la wakimbizi duniani, UNHCR, bwana Ruud Lubbers.
Kiongozi wa shirika la wakimbizi duniani, UNHCR, bwana Ruud Lubbers.Picha: AP

Kiongozi wa shirika la wakimbizi duniani, UNHCR, bwana Ruud Lubbers, amesema Sudan inataka umoja wa mataifa ithibitishe kwamba wakimbizi elfu 190 wa Darfur wamerudi makwao kwa hiari.

Lubbers pia amesema kuwa mkataba wa amani unaocheleshwa na unaolenga kumaliza mapigano ya kikabila huko Darfur, hautawasaidia raia wa Darfur, ikiwa hakutakuwa na juhudi zozote za kutafuta amani na kumaliza vita hivyo vya miezi 19.

Umoja wa mataifa umekadiria watu wasiopungua milioni 1.5 wamelazimika kuyahama makazi yao, huku wakimbizi elfu 200 wakiishi katika kambi za wakimbizi katika nchi jirani ya Chad. Mzozo wa Darfur ni tatizo kubwa la kiutu kuwahi kutokea duniani na limetatiza viongozi wa ngazi za juu ulimwenguni.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Khartoum, Lubbers amesema makamu wa rais, Ali Osman Mohamed Taha, alimlalamikia kwamba jamii ya kimataifa haiamini ripoti iliyotolewa na serikali kuhusu kurudi kwa wakimbizi wa Darfur. Hivyo amemtaka Lubbers kuandamana naye kujionea mwenyewe wakimbizi hao waliorudi kwa hiari.

Baada ya miaka kadhaa ya machafuko kati ya makabila ya kiarabu na wakulima waafrika, wakipigania raslimali kidogo zilizoko Darfur, waasi walizusha upinzani mkali, wakiilaumu serikali ya Khartoum kwa kutolijali eneo hilo na kuwasaidia wanamgambo wa kiarabu wa janjaweed katika mauaji yao ya safisha safisha na uporaji mali katika vijiji vya waafrika.

Serikali ya Sudan imekiri iliwapa silaha wanamgambo nchini humo kukabiliana na waasi, lakini imepinga kuwa na uhusiano na wanamgambo hao wa janjaweed. Azimio la baraza la usalama la umoja wa mataifa linatishia kuiwekea vikwazo Sudan, ikiwa itashindwa kumaliza mauaji ya Darfur, ambayo Marekani imesema ni mauaji ya halaiki.

Afisa wa wizara ya ulinzi ya Marekani aliye mjini Khartoum, amesema makundi yote yanayohusika katika vita hivyo lazima yapokonywe silaha, wala sio wanamgambo wa janjaweed pekee. Ameongeza kusema kwa sasa hali ya Darfur bado haijakuwa shuari, na akaonya huenda raia wengine elfu 100 wakimbilie nchini Chad kujiepusha na ghasia zinazoendelea. Ameeleza hofu yake kwamba baadhi ya wakimbizi huenda wasirudi tena makwao.

Lubbers amesema mazungumzo ya amani yanayolenga kumaliza vita vya miongo miwili vya wenyewe kwa wenyewe kusini mwa Sudan, yaliyopangwa kufanyika tarehe 7 mwezi ujao, mjini Naivasha nchini Kenya, hayapaswi kukamilika kabla ya kumaliza mzozo wa Darfur. Mazungumzo ya kuleta amani Darfur yaliyofanyika mjini Abuja, Nigeria mapema mwezi huu, hayakufaulu na yamepangwa kufanyika tena tarehe 21 mwezi ujao.

Wawakilishi wa serikali ya Sudan na chama cha Sudan Peoples Liberation Movement, SPLM, wametoa wito kwa jamii ya kimataifa na wadhamini kuisaidia Sudan na kiasi cha dola milioni 300 zitakazosaidia raia wa Darfur. Viongozi hao wametoa wito huo wa pamoja katika mkutano huko mjini Oslo, Norway, kuhusu mahitaji ya misaada kwa nchi yao.

Kiongozi wa ujumbe wa serikali kwenye mkutano huo, Yahia Hussein Mohamed, amesema pesa hizi zitatumiwa kuwasaidia wakimbizi kurudi makwao, kutoa misaada ya kiutu inayohitajika kwa dharura na kufanyia ukarabati barabara zilizoharibiwa wakati wa vita ili kuboresha uchukuzi. Pesa hizo pia zitavisaidia vyombo vya habari kudumisha amani katika eneo la Darfur na kuiwezesha serikali kutoa huduma bora za afya.