1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yakataa kikosi cha Umoja wa Mataifa

8 Septemba 2024

Sudan imekataa wito wa Umoja wa Mataifa wa kutumwa "kikosi huru kisichoegemea upande wowote" kuwalinda mamilioni ya raia waliolazimika kuyakimbia makaazi yao kutokana na vita vinavyoendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

https://p.dw.com/p/4kP86
Sudan | Abdel Fattah Al-Burhan
Kiongozi wa kijeshi wa Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.Picha: Sudanese Army/AFP

Vita hivyo vilivyoanza mwezi Aprili mwaka jana kati ya jeshi rasmi na wanamgambo wa Kikosi cha Dharura (RSF) vimepoteza maisha ya maelfu ya watu na kusababisha mojawapo ya majanga mabaya kabisa ya kibinaadamu kuwahi kushuhudiwa kwa miaka ya karibuni.

Wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa walisema siku ya Ijumaa (Septemba 6) kwamba kikosi chao cha kusaka ukweli kilikuwa kimegunduwa matukio ya "kutisha" ya uvunjaji wa haki za binaadamu unaofanywa na pande zote mbili, "ambao unalingana na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu."

Soma zaidi: Museveni na Jumuiya ya IGAD wajiingiza kwenye usuluhishi wa mzozo nchini Sudan

Wataalamu hao wametowa wito wa "kikosi huru na kisichoegemea upande wowote chenye jukumu la kuwalinda raia" kutumwa nchini Sudan bila kuchelewa."

Baadhi ya wakimbizi wa Sudan na Sudan Kusini waliokimbia vita nchini Sudan.
Baadhi ya wakimbizi wa Sudan na Sudan Kusini waliokimbia vita nchini Sudan.Picha: LUIS TATO/AFP

Wizara ya mambo ya nje ya Sudan, ambayo iko chini ya jeshi linaloendeswa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ilisema kwenye taarifa yake ya siku ya Jumamosi (Septemba 7) kwamba "serikali ya Sudan inakataa mapendekezo yote ya kuwa na kikosi cha Umoja wa Mataifa."

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa wapendekeza kupelekwa kikosi cha amani Sudan

Badala yake, serikali ya Sudan ililiita Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa, ambalo liliunda timu ya kusaka ukweli mwaka jana, kuwa ni "chombo cha kisiasa na kisicho uhalali", na ilisema mapendekezo ya kikosi hicho "yanakwenda kinyume kabisa na majukumu yake."

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa walisema raia milioni nane wamelazimika kuyakimbia makaazi yao na kugeuka kuwa wakimbizi wa ndani huku wengine milioni mbili wamekimbilia nchi za jirani.

Jeshi laituhumu RSF

Zaidi ya watu milioni 25, zaidi ya nusu ya raia wa nchi hiyo, wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula.

Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Sudan ilikituhumu Kikosi cha Dharura (RSF) kinachoongozwa na naibu wa zamani wa Burhan, Mohamed Hamdan Daglo, kwa "kuwalenga kwa makusudi raia na taasisi za kiraia."

Sudan | Mohamed Hamdan Daglo
Kiongozi wa waasi wa RSF, Jenerali Mohamed Hamdan Daglo.Picha: Ashraf Shazly/AFP

"Ulinzi wa raia unasalia kuwa kipaumbele cha juu kabisa cha serikali ya Sudan," ilisema taarifa hiyo.

Soma zaidi: Jeshi la Sudan 'lakubali kujiunga' na mazungumzo ya Geneva

Mbali na kukataa wito wa timu ya wataalamu ya kuwekwa marufuku ya silaha dhidi ya Sudan, taarifa hiyo iliongeza pia kwamba jukumu la Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa ni kusaidia mchakato wa kitaifa, badala ya kusaka njia ya kuleta mifumo ya nje kuingilia mambo ya ndani."

Hayo yanajiri wakati familia kadhaa zikikimbia viunga vya kaskazini vya mji mkuu wa Sudan, Khartoum, siku ya Jumamosi baada ya mapambano kupamba moto kati ya pande hasimu karibu na kituo muhimu cha kijeshi. Wapiganaji wa RSF wakiivamia kambi ya kijeshi ya Hattab kaskazini mwa Khartoum tangu siku ya Jumatano. 

Vyanzo: AFP, Reuters