1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Spika azuia mjadala kuhusu mkataba wa bandari ya Tanzania

Deo Kaji Makomba
29 Agosti 2023

Spika Tulia Ackson wa Tanzania, amezuia mjadala juu ya mkataba wa bandari baina ya serikali ya Tanzania na kampuni ya DP World ya Dubai kujadiliwa Bungeni ikiwa tayari Bunge hilo limeishamaliza majukumu yake ya awali.

https://p.dw.com/p/4Vi5D
Spika wa bunge la Tanzania Dr. Tulia Ackson
Spika wa bunge la Tanzania Dr. Tulia AcksonPicha: Ericky Boniphace

Dr. Tulia Ackson, spika wa bunge la Tanzania,  amesema suala hilo linaweza kujadiliwa endapo litaletwa katika utaratibu mwingine wa kibunge. 

Spika Tulia ametoa kauli hiyo hii leo muda mfupi baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu ya wabunge katika mkutano wa 12 wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililoanza vikao vyake hii leo jijini Dodoma.

Amesema kuwa Bunge lilishamaliza mjadala huo hivyo wabunge wanatakiwa kuendelea kuwasikiliza wananchi.

Hata hivyo kauli hiyo ya Spika wa bunge la Tanzania imepokelewa kwa hisia mseto na wachambuzi wa siasa nchini Tanzania, baadhi wakisema kuwa kauli hiyo inachora msitari na kujaribu kuzuia mjadala huo kuhusiana na mkataba wa Bandari baina ya serikali ya Tanzania na kampuni ya DP World ya Dubai. 

Tanzania kufanyia kazi mapendekezo mkataba wa DP World

Kauli hiyo ya Spika wa Bunge la Tanzania inakuja huku mjadala ukiendelea kuhusiana na suala hilo ukihusisha wanasiasa, wanasheria, wanaharakati, viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla, hasa mara baada ya bunge hilo katika mkutano wake wa 11 kupitisha makubaliano ya mpango wa Serikali ya Tanzania katika kuingia makubaliano na kampuni ya DP World ya Dubai ili kuendesha bandari za Tanzania.