1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SPD,Kijani na FDP waanza mazungumzo rasmi

7 Oktoba 2021

Itakuwa mara ya kwanza Ujerumani kuongozwa na serikali ya mseto kati ya SPD,Wanamazingira na Waliberali ikiwa vyama hivyo vitaunda serikali

https://p.dw.com/p/41PFK
Deutschland | Live-Talk zur Energie- und Klimapolitik in Berlin | Christian Lindner, Annalena Baerbock und Olaf Scholz
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Nchini Ujerumani chama cha Social Democratic-SPD hii leo kimeanza mazungumzo rasmi ya kwanza na vyama vidogo vya Kijani na Free Democrats FDP,yakiwepo matumaini kwamba vyama hivyo vinaweza kupiga hatua, hatimae kuunda serikali mpya ya mseto.

Chama kilichopata ushindi katika uchaguzi wa mwezi Septemba nchini Ujerumani cha Social Democratic SPD, kimeeleza kuwa na matumaini katika siku ya mwanzo ya duru yake ya kwanza ya mazungumzo rasmi ya kutafuta maelewano ya kuunda serikali na vyama viwili vidogo.

Jana Jumatano chama cha Kijani cha wanamazingira na Waliberali-Free Democratic FDP walikubaliana  kuingia kwenye mazungumzo na SPD ambacho kilifanikiwa kwa wingi mdogo kuishinda kambi ya wahafidhina ya Kansela Angela Merkel anayeondoka madarakani. Baada ya kikao chao na FDP kiongozi wa wanamazingira Annalena Baerbock aliweka wazi mwafaka waliofikia pamoja.

"Baada ya mazungumzo haya tumeshauriana na kila mmoja na kufikia mwafaka kwamba inaingia zaidi akilini hivi sasa kuingia kwenye mazungumzo ya kina pamoja na FDP na SPD na hususan kwa mtazamo wa kutafuta msimamo wa pamoja ambao tumeweza kuuanzisha kwenye mazungumzo yetu ya pande mbili''

Deutschland | Live-Talk zur Energie- und Klimapolitik in Berlin | Kanzlerkandidaten
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Hii leo Alhamisi naibu kiongozi wa SPD Norbert Walter-Borjans amesema mazungumzo ya pande tatu yatakwenda moja kwa moja kwenye hatua ya kushughulikia kuzitatua tafauti zilizopo, moja baada ya nyingine kwa mtazamo wa kuunda serikali ya mseto iliyopewa jina la taa za trafiki kutokana na rangi za alama za vyama vitatu, Kijani, Njano na Nyekundu.

Vyama vyote viwili vyenye kura ya turufu Kijani na FDP viliweka pembeni wazo la kuzungumza na kambi ya wahafidhina lakini jana Jumatano walisema hakutokuweko mazungumzo mengine ya pembeni kwa hivi sasa. Kiongozi wa FDP Christian Lindner alisema chama chake kina sera zinazokubaliana na kambi ya wahafidhina lakini kimefikia makubaliano ya pamoja na wanamazingira kwamba nchi hii inapaswa kuwa na mwelekeo mpya.

Uamuazi huo umeonesha kutuma ujumbe wa wazi kwa kambi ya wahafidhina kama alivyosikika akiweka wazi Markus Söder kiongozi wa CSU:

''Hatimae tumepata picha kamili, leo chama cha Kijani na FDP vimetupa msimamo wa wazi na kukataa serikali ya Jamaica. Tumesikitishwa sana na Uamuzi huu''

Kwa hakika itakuwa ni mara ya kwanza kushuhudiwa nchini Ujerumani serikali ya mseto ya SPD, Wanamazingira na Waliberali FDP katika ngazi ya shirikisho ikiwa vyama hivyo vitaunda serikali, ingawa serikali kama hiyo ipo katika jimbo la Rhineland Palatinate, magharibi mwa Ujerumani.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW