1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Spain yaipiku Italia kusonga mbele EURO 2024

Josephat Charo
21 Juni 2024

Uhispania wamefanikiwa kufuzu kwa raundi ya mtoano ya timu 16 bora katika michuano ya kombe la EURO 2024 baada ya kuwachapa mabingwa watetezi Italia 1-0.

https://p.dw.com/p/4hKqS
Alvaro Morata wa Uhispania akishangilia baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Italia
Alvaro Morata wa Uhispania akishangilia baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Italia Gelsenkirchen 20.06.2024Picha: JESPER ZERMAN/BILDBYRÅN/picture alliance

Uhispania imefuzu kwa duru ya mtoano ya timu 16 bora katika michuano ya kombe la EURO 2024 kwa kuichapa Italia 1-0 katika mechi ngumu ya kundi B. Ushindi huo wa bao la pekee la Riccardo Calafiori dakika 10 baada ya kupindi cha pili kuanza una maana Uhispania inajiunga na wenyeji Ujerumani katika duru ya mtoano ikiwa bado na mechi moja ya makundi.

Croatia na Albania zilitoka sare 2-2 katika mechi nyingine ya kundi hilo siku ya Jumatano kwa hiyo Italia bado wangali katika nafasi ya pili kwa ushindi wao wa 2-1 walioupata dhidi ya Albania mechi yao ya ufunguzi.

England ilipata tabu sana kudhihirisha uwezo wao wa kushinda kombe la EURO 2024 ilipolazamishwa sare 1-1 na Denmark katika mechi ya kundi C. Matokeo haya yanaiweka England katika mtihani mgumu kuhakikisha wanasonga mbele katika duru ya mtoano. Ushindi kwao ungewewazesha kufuzu kama washindi wa kundi C baada ya ushindi wa 1-0 walioupata dhidi ya Serbia mechi yao ya ufunguzi.

Hata hivyo mchezo wa kiwango cha kutoridhisha wa vijana wa kocha Gareth Southgate umeibua maswali mengi kuhusu kampeni yao ya kutaka kuwa mabingwa wa Ulaya kwa mara ya kwanza. Southgate amesema changamoto ni kufanya jambo ambalo halijawahi kufanywa hapo kabla.

"Naam tunahitaji kuangalia, ni wazi tumevunjika moyo na kiwango cha mchezo tulioonesha katika mechi zetu mbili. Tunahitaji kwenda na kuchambua kwa kina na tutafute njia kadhaa za kusuluhisha na kushughulikia mapungufu tuliyonayo. Katika siku chache zijazo, tutatumia muda mwingi kulifanyia kazi suala hilo."

Morten Hjulmand wa Denmark akishangilia na wachezaji wenzake baada ya kusawazisha dhidi ya England
Morten Hjulmand wa Denmark akishangilia na wachezaji wenzake baada ya kusawazisha dhidi ya EnglandPicha: REUTERS

Kocha wa England Gareth Southgate aliongeza kusema, "Tunafahamu kiwango kinatakiwa kuwa juu. Tunajua kiwango kinaweza kuwa cha juu. Pengine jambo kubwa muhimu tunatakiwa kuyakubali mazingira tulimo na matarajio yanayotuzunguka. Na tutalazimika kufanya kazi kuishughulikia changamoto hiyo. Kwa sasa tumepungukiwa kidogo katika hilo. Mimi ndimi kocha na hili ni jukumu langu na natakiwa kukiongoza kikosi hiki katika njia nzuri kabisa kadri inavyowezekana kupata matokeo yasiyo ya kawaida."

Denmark hawajavunjika moyo

Denmark walishambulia na kucheza vizuri zaidi kuliko England na walionekana wakicheza kwa mshikamano zaidi, baada ya kufungua mashindano haya ya EURO kwa sare ya 1-1 dhidi ya Slovenia.

Kocha mkuu wa Denmark, Kasper Hjulmand, alisema, "Siwezi kusema tumevunjika moyo lakini ni aibu. Kuna matokeo ambayo tungeyapata lakini siwezi kusema tumevunjika moyo kwa sababu tumefanya vyema. Tulikuwa na hisia nzuri kuhusu mchezo huu na tuliamini tungeshinda. Nafikiri tumecheza vizuri lakini jambo la muhimu sana kwangu mimi ni kwamba tumecheza jinsi tulivyocheza leo. Katika mechi zijazo tunaweza kushinda au tupoteze, lakini kucheza namna hii, kama tulivyocheza leo, ndilo jambo la muhimu zaidi."

Soma pia: Ujerumani yawa ya kwanza kufuzu duru ya mtoano EURO 2024

Katika mechi nyingine ya kundi C Luka Jovic wa Serbia alifunga bao katika muda wa mazdadi kulazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Slovenia.

England inaongoza kundi C na alama nne na iko katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwa hatua ya 16 bora. Mechi za mwisho za kundi C zitachezwa Jumanne wiki ijayo huku England ikimenyana na Slovenia na Denmark ikivaana na Serbia.

Mechi tatu zinachezwa leo Slovakia ikiwa na miadi na Ukraine katika kundi E na Poland ikimenyana na Austria katika kundi D. Usiku Uholanzi itapambana na Ufaransa katika mechi nyingine ya kundi D.

(afpe, dpa)