1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SILAHA NDOGO NDOGO ZASABABISHA MAAFA MAKUBWA

Mohamed Dahman11 Julai 2005

Wahanga wengi wa vita siku hizi wanakufa kutokana na silaha ndogo ndogo kama vile bunduki za rashasha,bastola na bunduki za kawaida na kuzifanya silaha hizo kuwa silaha hasa zenye kuleta maanganizi makubwa ya binaadamu duniani leo hii.

https://p.dw.com/p/CEFe

Repoti hiyo ambayo ni uchunguzi wa karibuni kabisa wa kila mwaka juu ya silaha ndogo ndogo uliofanywa na watafiti katika Taasisi ya Wahitimu ya Masomo ya Kimataifa ilioko mjini Geneva imesema kwamba vifo vya migogoro vilivyosababishwa na matumizi ya silaha ndogo ndogo idadi yake huko nyuma imekuwa ikiripotiwa kwa kiasi cha chini mno.

Kwa mfano idadi ya wahanga waliokufa moja kwa moja kutokana na kushambuliwa na silaha hizo yumkini ikafikia 80,000 hadi 108,000 kwa mwaka 2003 ikilinganishwa na makadirio yaliotolewa awali na watafiti wengine kwamba ilikuwa kati ya 27,000 hadi 51,000 kwa mwaka huo.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo makadirio hayo ya chini kwa kiasi kikubwa yametokana na uchache wa data halisi na wachambuzi kutegemea mno makadirio ya maelezo ya serikali na vyombo vya habari kuhusu vita ambayo mara nyingi yanakuwa sio sahihi.

Idadi ya vifo visivyotokana moja kwa moja na silaha ndogo ndogo ambavyo silaha hizo zinaweza kulaumiwa pia zimekadiriwa vibaya na silaha za aina hiyo ndio sasa zinazochochea uharibifu mkubwa wa kijamii ambao husababisha utapia mlo,njaa na vifo kutokana na maradhi yanayoweza kuzuilika.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo kutegemea na umbile la mzozo silaha ndogo ndogo husababisha kati ya asilimia 60 hadi 90 ya vifo vinavyotokana moja kwa moja na vita.

Kwa kuzingatia utaratibu uliobuniwa na Umoja wa Mataifa silaha ndogo ndogo ni kuanzia bastola na bunduki hadi bunduki za rashasha za kijeshi,mizinga midogo na makombora yanayoweza kubebwa mkononi ya kudungulia vifaru.

Umoja wa Mataifa ulipitisha mpango wa utekelezaji hapo mwaka 2001 kutokomeza biashara haramu ya silaha ndogo ndogo duniani na uchunguzi huu wa hivi karibuni unakwenda sambamba na kufunguliwa kwa mkutano wa juma moja wa Umoja wa Mataifa leo hii/hapo jana unaokusudia kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa mpango huo.

Mwenyekiti wa mkutano huo balozi wa Finland kwenye Umoja wa Mataifa Pasi Patokallio amesema hizi ndio silaha halisi za maangamizi ya umma.

Balozi huyo ameendelea kusema kwamba wakati nadhari kubwa ya dunia iko juu ya uwezekano wa maangamizi makubwa ya silaha za kibaolojia,kemikali na nuklea silaha nyepesi ambazo zinaweza kubebwa na mtu mmoja tu zinahusika na umwagaji mkubwa wa damu katika vita hivi leo .

Uchunguzi huo unaofanyika kila mwaka kuanzia mwaka 2001 umekadiria kwamba biashara halali ya kimataifa ya jumla katika silaha ndogo ndogo kuwa dola bilioni 4 kwa mwaka na ile ya haramu kuwa chini ya dola bilioni moja kwa mwaka wakati nchi nyingi hazitowi data za kuingiza na kusafirisha nje silaha.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo migogoro mara nyingi inachochewa duniani kote kutokana na kupatikana kwa urahisi kwa silaha ndogo ndogo.Kwa mfano akiba kubwa ya silaha hizo ilioko nchini Afghanistan na Iraq imetowa changamoto kubwa kwa Marekani na washirika wake wakipigania kuleta usalama na utulivu wa kisiasa.

Hata hivyo baadhi ya nchi zimefanikiwa sana kusalimisha silaha za watu wake kwa msingi wa kufanya hivyo kwa hiari ili kupunguza idadi ya vifo na kuongeza utulivu.

Serikali ya Brazil ikishtushwa kutokana na kuongezeka kwa raia wanaopoteza maisha kwa silaha hizo imezitia mkononi zaidi ya silaha hizo 300,000 kwa kupitia mpango wa kuwashajiisha watu wazisalimishe kwa hiari.Nchi hiyo wiki iliopita pia ilipitisha muswada wenye kuidhinisha kura ya maoni hapo tarehe 23 mwezi wa Oktoba juu ya ama au la kupiga marufuku mauzo ya silaha nchini kote.

Lakini huko Mashariki ya Kati kuliko tete kutokana na mzozo wa muda mrefu kumiliki silaha kumezagaa na inaonekana kuongezeka ambapo uchunguzi huo unakadiria kwamba silaha ndogo ndogo zinazofikia milioni 45 hadi milioni 90 ziko mikononi mwa raia.

Silaha zinazomilikiwa kinyume na sheria pia zinatishia usalama wa umma huko Afrika ya Kati na Afrika Mashariki kwa kuchochea uhalifu na kurefusha migororo.

Wakati Marekani,Italia,Brazil,Ujerumani na Ubelgiji zinatajwa kuwa wasafirishaji wakubwa wa silaha duniani idadi kubwa ya silaha kutoka maeneo ya Balkan na Ulaya ya mashariki zinamiminika katika nchi za maziwa makuu licha ya kuwepo kwa ushahidi kwamba zinatumika kwenye ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu.Katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo watu wenye silaha bado wanaendelea kubaka,kupora na kuuwa raia.