1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya kupambana na ujinga duniani

Mitima DelaChance8 Septemba 2023

Dunia inaadhimisha siku ya kupambana na ujinga wiki hii. Nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo takwimu zinaonyesha kuwa 29% ya wakongo hawajui kusoma na kuandika.

https://p.dw.com/p/4W6dm
Ghana House of Grace School for the Deaf students
Picha: Penplusbytes

Takwimu hizo za miaka mitatu iliyopita zinaonyesha pia kwamba wengi kati ya wakongo wasiojuwa kusoma na kuandika ni wanawake kwa asilimia arobaini (40%). Ili kurekebisha hali hii, tangu mwaka 2012, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imeunda mkakati wa kupambana na hali hiyo, ili  kupunguza kiwango cha watu wasiojua kusoma na kuandika  kwa angalau 10% kila mwaka. Hayo ni katika dhamira ya kutekeleza ahadi zake za kitaifa na kimataifa katika kutokomeza hali hiyo ifikapo mwaka 2030.

Serikali ya Kongo imeanzisha  pia baadhi ya vituo vya mafunzo ya kusoma na kuandika, lakini pia kuna mipango ya kibinafsi kote nchini ambayo inalenga kuwaelimisha watu wazima kusoma na kuandika. Gorette Bulangalire ni mwanamke mwenye umri wa angalau 65, licha ya kuwa na majukumu ya familia, ameamua kujifunza kusoma na kuandika.

Indonesien Humor Literatur
VitabuPicha: IHIK3

Kuandaa programu za kusoma na kuandika kwa watu wazima ni pendekezo lililopo kwa zaidi ya miongo mitatu nchini Kongo. Tayari ripoti ya Tume ya Elimu ya Mkutano Mkuu wa Kitaifa ulioandaliwa mnamo mwaka 1992 ilikuwa imependekeza kuundwa mifumo ya kupambana na tatizo la kutojua kusoma na kuandika kote nchini humo wakati ule ilipokuwa ikiitwa Zaire.

Vile vile, kifungu cha 44 cha katiba mpya ya DRC kinabaini kwamba kutokomeza hali ya watu  kutojua kusoma na kuandika  ni jukumu la kitaifa kwa mafanikio ambayo serikali inapaswa kuandaa programu maalum. 

Isaac Bishamamba ni mwalimu wa kiswahili na pia mmiliki wa kituo kinaochoitwa Kazi Maendeleo kilichobobea katika kutoa mafunzo ya kusoma na kuandika kwa watu wazima mjini Bukavu. Ameelezea mafanikio na changamoto wanazokabiliana nazo.

Soma pia: UNESCO yasema watoto milioni 250 duniani hawajui kusoma na kuandika

Alipofika madarakani mnamo mwaka 2018, Rais Félix Tshisekedi alionyesha dhamira ya kupambana na kutoelimishwa akisisitiza nia yake ya kuboresha sekta ndogo ya elimu isiyo rasmi na suala la kujua kusoma na kuandika.

Felix Tshisekedi Präsident DR Kongo
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Félix TshisekediPicha: Isa Terli /AA/picture alliance

Serikali ya Kongo imetangaza elimu ya bure katika shule ya msingi, jambo lililochangia kwa kiwango fulani kupambana dhidi ya hali ya kutojua kusoma na kuandika, kama alivyoeleza Gilbert Bwalibuduge ni Mkaguzi wa elimu ya msingi, sekondari mjini Bukavu.

Katika taarifa ya hivi karibuni, Naibu waziri Mkuu anaehusika na utumishi wa Umma Jean-Pierre Lihau Ebue aliwapongeza wale wote ambao jukumu lao la kila siku bila kuchoka ni kufuta ujinga kwa wananchi wenzao ambao hawajapata nafasi ya kupata elimu na maarifa kwa wakati muafaka.

(Imeandaliwa na Mitima Delachance, DW, Bukavu)

Mhariri: Iddi Ssessanga