1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya kimataifa ya wahamaji: mchango wa wahamiaji duniani

RM17 Desemba 2004

Yapata watu milioni 180 wanaishi katika nchi za mbali na walikozaliwa: Hii ni idadi kubwa kabisa katika historia ya binadamu. Sehemu ndogo tu kati ya watu hawa, yapata watu milioni 20 tu, ndiyo haswa wakimbizi. Lakini uhamiaji upo tangu miaka mingi iliyopita – japo siyo kwa kiwango kikubwa kama hivi sasa. Ongezeko la uhamiaji duniani linatokana na wimbi la utandawazi. Tangu mwaka 2003 umoja wa mataifa kwa kutumia azimio lake maalumu, unajaribu kutoa haki za kisheria kwa wahamiaji.

https://p.dw.com/p/CHhz
Wahamiaji kutoka Uturuki nchini Ujerumani wakisali kwenye msikiti wa Berlin
Wahamiaji kutoka Uturuki nchini Ujerumani wakisali kwenye msikiti wa BerlinPicha: AP

Mataifa 27 tu ndiyo yamepitisha rasmi azimio la Umoja wa mataifa kuhusu wahamiaji, na nchi nyingine 15 zimeweka saini. Hata hivyo kati ya mataifa yaliyoafikiana na azimio hili, hakuna nchi hata moja kutoka katika nchi za viwanda. Hali hii inaonyesha wazi jinsi wahamiaji wanavyovyaswa, hata katika nchi za Ulaya na Marekani ambako wahamiaji milioni 100 wanaishi. Lakini ukweli wa mambo kwamba, watu milioni 180 ni wahamiaji – sawa na asilimia 3 ya idadi ya wakazi duniani --- hauwezi kufichika kirahisi. Hata kama wahamiaji wengi wanafanya kazi ngumu huku wakiishi maisha magumu katika nchi tajiri -- kwenye vitongoji vya Kalkutta-India, New-York, London au nchi za utajiri wa mafuta kwenye eneo la Ghuba.

Saa nyingine wahamiaji hukaribishwa kwa mikono miwili, kwa mfano Marekani, lakini kwa vigezo tete: wanaokaribishwa ni watu walio na elimu nzuri, wafanya biashara wa hali ya juu na hasahasa wenye ngozi nyeupe.

Wakati kelele nyingi hivi sasa zinawalenga wahamiaji kutoka nchi za kusini kwenye nchi za viwanda, wakaazi wa nchi za viwanda kwa mfano Marekani, wanasahau kuwa wao nao walihamia tu Marekani, sawa na wahamiaji wapya wa leo. Wahamiaji wanatoa mchango mkubwa wa maendeleo ya kiuchumi na kiutamaduni. Wahamiaji huja na fikra mpya na mbinu mpya kwenye jamii.

Kwa upande mwingine uhamiajiwa nyakati za leo unaonekana kuwa muhimu sana kwa nchi za viwanda na uchumi duniani, kwani wahamiaji ndiyo wanaofanyishwa kazi kama mashine. Tabaka la juu katika nchi za kiarabu, wanawatumia wahamiaji kwa kazi ngumu za kila aina – kwani hawa ndiyo wanaweza kuwaajiri leo na kuesho kuwafukuza.

Pamoja na kazi ngumu kwenye mazingira magumu, wahamiaji siyo mashine, hawa ni watu wanaotumia nafasi hii kutoa mchango mkuwa kwa ndugu zao katika nchi walikotoka. Wahamiaji wanatuma mabilioni ya fedha kwenye walikotoka. Fedha hizi zinatoa pia mchango wa maendeleo duniani.

Kwa mantiki hii wahamiaji wanatoa mchango mkubwa duniani katika maendeleo ya kiuchumi na kiutamaduni – wanatumiwa kwenye majeshi ya ulinzi, kufanya kazi ngumu, lakini ni mabalozi pia wa fikra na mawazo mapya.

Azimio la Umoja wa mataifa juu ya wahamiaji linajaribu kutoa haki za kisheria kwa wahamiaji. Hii ni hatua ndogo tu, lakini ni mwanzo mzuri wa kuwalinda wahamiaji. Na ni mwanzo mzuri wa kuanza kuwafumbua macho walimwengu, watambue na kuenzi mchango wa wahamiaji duniani kote.