Siasa za Kimataifa za Ujerumani zilibadilika chini ya utawala wa vyama vya SPD na Kijani
28 Julai 2005Kambi ya kujihami ya nchi za Magharibi, NATO, iliamua kupeleka majeshi yake ili kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe, na kuleta amani, katika nchi za Balkan. NATO iliitaka Ujerumani, ambayo ilikuwa mwanachama, pia ipeleke majeshi yake.
Hadi wakati huo, majeshi ya Ujerumani yalikuwa hayajashiriki katika vita vyoyyote nje ya nchi hiyo, tangu mwisho wa vita vikuu vya pili vya dunia.
Kutokana na mikataba ya amani nchi hiyo iliyosaini mwisho wa vita hivyo, kulikuwa na vipengele vilivyoweka masharti magumu kwa jeshi la Ujerumani kuhusika katika vita, nje ya nchi.
Waziri wa Mambo ya Nje, Joschka Fischer, wa chama cha Kijani ambacho kilikuwa kinajihusisha sana na masuala ya kuleta amani duniani, alitaka na alikuwa na uwezo wa kukubali wito huo wa NATO.
Kutokana na matukio hayo, ukurasa mpya wa siasa za Kijerumani za masuala ya kimataifa na usalama ukaanza.
Waziri Fischer, akielezea kuhusu wakati huo, alisema:
“Tuliitwa kwenye ofisi za Kansela, kwa mara ya kwanza tangu kuundwa kwa Shirikisho la Jamhuri la Ujerumani ilibidi tufanye maamuzi juu ya vita na amani. Maamuzi hayo kwetu sisi yalikuwa magumu.”
Waziri Fischer ni waziri wa kwanza wa Mambo ya Nje, kutoka chama cha Kijani, katika historia ya Ujerumani. Yeye, pamoja na chama chake, wangependa kushughulikia masuala ya kisiasa kupitia amani kwanza, badala ya vita.
Lakini serikali na bunge la Ujerumani wakaamua kushiriki katika kampeni za kivita na NATO. Walishiriki kwenye mashambulizi ya ndege za kivita dhidi ya Yugoslavia, yalioanza mwezi Machi, 1999.
Ndege za kivita za Ujerumani, aina ya Tornado, zikatumwa vitani na serikali ya muungano wa vyama vya SPD na Kijani.
Wanachama wenzake Waziri Fischer, kutoka chama cha kijani, hawakufurahishwa na maamuzi haya. Mkutano wa dharura wa chama ukaitwa kujadili suala hili na wanachama wengi kwenye mkutano huo walionyesha kutopendezwa na uamuzi wa serikali.
Msimamo wa wakati huo wa Waziri Fischer ni kwamba mashambulio ya mabomu ya majeshi ya NATO yasingeweza kuleta matoke mazuri. Kwa mtazamo wake, yangemfanya Slobodan Milosevic, kiongozi wa Yogoslavia wa wakati huo, kuungwa mkono zaidi.
Kwa sababu alikuwa na msimao huu, Waziri Fischer alirushiwa usoni mfuko wenye rangi. Lakini aliendelea kutetea utumiaji wa nguvu uwe chagua la mwisho katika masuala ya kisiasa.
Serikali ya Ujerumani ilikuwa imefikia uamuzi ambao ilibidi kila mara inapouhitaji, kuurudia na kuutathmini upya. Baada ya mashambulio ya kigaidi dhidi ya Marekani, kwenye miji ya New York na Washington, mwezi Septemba mwaka 2001, Kansela Gerhard Schröeder alisema:
“Huu ni wito wa vita dhidi ya nchi zote duniani zilizoendelea katika demokrasia. Atakaye wasaidia au kuwalinda magaidi hawa, anaenda kinyume na maadili yote ya kuishi kwa amani baina ya binadamu. Wananchi wa Ujerumani wana waunga mkono Wamarekani katika kipindi hichi ambacho ni kigumu sana kwao.”
Tukio hili lilimaanisha kwamba jeshi la Ujerumani, kwa mara nyingine tena, litashiriki katika mapigano nje ya nchi yake. Wakati huo ilimaanisha dhidi ya Taliban na mtandao wa kikundi cha kigaidi cha Al Qaeda, nchini Afghanistan.
Lakini kama ilivyo kawaida katika suala la kupeleka jeshi lake nje, ilibidi Bunge la Ujerumani lipige kura. Baadhi ya wanachama wa vyama vya SPD na Kijani hawakupiga kura. Ikambidi Kansela Schröeder aingilie kati.
Akaunganisha kura hiyo na kura ya kuwa na imani naye, na akaweza kupata kura nyingi zinazounga mkono operesheni hiyo ya kivita iliyoshirikisha majeshi ya Marekani, operesheni iliyojulikana kama ‘Enduring Freedom’.