1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SHIRIKA LA MAZINGIRA LA UMOJA WA MATAIFA NA TSUNAMI

7 Januari 2005

Athari za zilzala iliyoshambulia katika eneo la Bahari ya Hindi imelifanya Shirika la Umoja wa Mataifa lizipe umbele harakati za kuunda mfumo wa kuonya mapema katika eneo hilo. Habari hiyo ilitangazwa na Klaus Töfper, Mkurugenzi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa wakati akihudhuria Mkutano wa Kimataifa mjini London kuhusu mustakabali wa mataifa ya visiwa katika maeneo yenye kuhitaji maendeleo. Kwanza watu wa eneo hilo watahitaji kupatiwa misaada ya kuikarabati hasara ya kiuchumi iliyosababishwa na Tsunami. Kisha hapo patakuweko mahitaji ya kukichunguza kiwango cha hasara kilichotiwa katika mazingira na maafa ya mafuriko ya maji, alisema Bwana Töpfer.

https://p.dw.com/p/CHhr

Kwa muda mrefu mjini London ilikwisha pangwa tarehe ya mkutano wa waandishi wa habari wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP. Hata hivyo maafa ya mafuriko ya maji huko Asia yamezidi kusisitiza umuhimu wa uchunguzi kuhusu vitisho vya kimazingira vinavyoyakabili mataifa ya visiwa, ambavyo vilikuwa mada ya mkutano huo. Ndiyo maana kwa sasa Umoja wa Mataifa umeupa umbele muundo wa mfumo wa kuonya mapema dhidi ya vitisho vya Tsunami, alisema Mkurugenzi wa UNEP, Klaus Töpfer. Hata hivyo kwa sasa hakuweza kukadiria gharama za mfumo kama huo wa kuonya mapema. Benki ya Maendeleo ya Asia, alisema, imo njiani kugharimia uchunguzi kuhusu kipimo kinachowezekana cha gharama hizo. Wakati huo huo Bwana Klaus Töpfer alikaribisha ile imani kubwa ya watu ya kutoa michango ya hali na mali kwa wahanga wa maafa hayo.

Alisema misaada hiyo mingi ya kibinafsi ya pesa pamoja na misaada mikubwa ya kiserikali inahitaji halahala ili kusaidia moja kwa moja hivi sasa pamoja na kutunga mipango ya usaidizi wa muda mrefu kwa nchi zilizoathirika.

Mkuu huyo wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa alizungumza pia juu ya umuhimu wa kuchunguzwa kwa makini kipimo cha hasara ya mazingira kilichosababishwa na Tsunami. Miradi yoyote ya ukarabati itabidi kuzingatia umuhimu wa kuhifadhiwa mwambao zenye matumbawe, misitu ya mikoko na sehemu nyingine ambazo ni tete kwa mazingira ya maeneo yaliyokumbwa na maafa. Bwana Töpfer alisema kuwa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa limekwisha peleka mabingwa wake katika nchi mbali mbali za maafa.

Anasema kuwa wafanya kazi wake wako tayari Indonesia, Sri Lanka, maldieves na Thailand wakihitajiwa huko kwa harakati za dharura. Pia alisema kuwa Indonesia inatatumaini itaweza kuwekewa Kituo cha Maafa ya Mazingira, yaani Environment Desaster Center kitakacholihudumia eneo zima. Kisha akasisitiza kuwa wanakabiliwa na kazi kubwa ya kusafisha taka uchafuzi na taka zilizosababishwa na mawimbi makali, uchafu ambao unaleta kitisho kikubwa kwa afya ya watu.

Mkuu huyo wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa hakuona umuhimu wa kutafutwa wa kulaumiwa kwa maafa ambayo yamesababisha vifo zaidi ya laki moja na nusu.