1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shireen wa Aljazeera kuzikwa Jerusalem

13 Mei 2022

Israel yapeleka jeshi la ziada Jerusalem kuzuia machafuko wakati wa maziko ya mwandishi habari wa Aljazeera aliyeuwawa kwa kupigwa risasi akiwa kazini

https://p.dw.com/p/4BFa0
Trauer um Shireen Abu Akleh | Palästina
Picha: Al Jazeera/dpa/picture alliance

Israel imeimarisha hali ya usalama katika mji wa Jerusalem kabla ya maziko ya mwandishi habari wa kituo cha televisheni cha Aljazeera Shireen Abu Akleh aliyeuwawa kwa kupigwa risasi.

Mwandishi habari wa siku nyingi wa Aljazeera Shireen Abu Akleh anazikwa leo ijumaa siku mbili baada ya kuuliwa kwa kupigwa risasi wakati wa msako uliofanywa na wanajeshi wa Israel. Israel na Palestina zimetupiana lawama kuhusiana na kifo  cha mwandishi huyo mwenye umri wa miaka 51 Mmarekani mwenye asili ya kipalestina,kilichotokana na kupigwa risasi kufuatia vurugu zilizozuka katika kambi ya wakimbizi ya Jenin.

Trauer um Shireen Abu Akleh | Rauch Flüchtlingslager Dschenin bei Zusammenstößen
Picha: JAAFAR ASHTIYEH/AFP

Mwili wa Abu Akleh ambaye alikuwa ni mkristo - aliyezaliwa Palestina, Jerusalem Mashariki eneo lililonyakuliwa na Israel,umehamishiwa katika mji huo mtakatifu kutoka Ukingo wa Magharibi.Jeneza lililoibeba maiti yake lilianza safari likisindikizwa na umati wa watu waliokuwa wakipiga kelele za kudai Palestina isitishe ushirikiano wa kiusalama na Israel.Msemaji wa jeshi la Israel ameliambia shirika la habari la AFP, maelfu ya waombolezaji wanatarajiwa kushiriki ibada ya mazishi katika kanisa la mji wa kale wa Jerusalem majira ya mchana.

Barabara zitafungwa katika eneo hilo na wanajeshi wa ziada wamepelekwa katika mji wa Jerusalem kuhakikisha  mazishi yanafanyika salama bila ya machafuko ambayo yanaweza kuhatarisha maisha ya wanaohudhuria au watu wengine.Kutokana na umaarufu wake jana Abu Akleh aliagwa katika shughuli rasmi ya kiserikali iliyofanyika katika uwanja wa ikulu ya rais Mahmoud Abbas mjini Ramallah.

Maelfu ya watu walijipanga msururu wakati jeneza lake likipitishwa katika Ukingo wa Magharibi likiwa limefunikwa bendera ya Palestina,na ambako pia barabara moja itapewa jina lake kumuenzi.Sheeren Abu Akleh alikuwa mwandishi habari aliyesifika kwa kiwango kikubwa kutokana na ushujaa na weledi katika kazi yake.Watu waliojitokeza kumuaga buriani walionekana wakiwa wamebeba mashada ya mauaa na picha za sura yake.Hadil Hamdan mmoja wa waombolezaji waliokuwa kwenye msururu wa kumuaga amesikika akisema sauti ya Sheerin ilisikika kila nyumba na kifo chake kimeziumiza nyoyo zao.

Marekani,Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa wameunga mkono miito inayotolewa ya kutaka uchunguzi kamili ufanyike kuhusu kile ambacho kituo cha Aljazeera imekiita mauaji ya makusudi ya kikatili lakini mamlaka ya Wapalestina imeshakataa kufanya uchunguzi wa pamoja na Israel.

Trauer um Shireen Abu Akleh | Ibrahim Almasri ägyptischer Fotograf
Picha: Mehmet Guzel/AP/picture alliance

Waziri mkuu wa Israel Naftali Bennet mara baada ya tukio alisema inawezekana Abu Akleh aliuwawa na risasi iliyofyetuliwa na wapalestina,na saa chache baade waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Benny Gantz akasema inawezekana ni Wapalestina waliompiga risasi au risasi ilitoka upande wa Israel.

Wakati akipigwa risasi hiyo Abu Akleh alikuwa akiripoti kutoka kambi ya Jenin akiwa amevalia kizibao cha kumkinga na risasi na ambacho kilikuwa na maandishi ya wazi kabisa yanayoonesha ni mwandishi wa habari,alikuwa pia na kofia ngumu kichwani. Kuuwawa kwake hakukuamsha majonzi Palestina tu lakini mpaka Uturuki, Sudan na kwengineko ambako yalizuka maandamano.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW