1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shinikizo laongezeka dhidi ya May

25 Machi 2019

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May aliwahi kuwadokeza wabunge wanaounga mkono Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya ama Brexit kuwa angeachia ngazi iwapo wangeyapigia kura makubaliano aliyoyafikia na Umoja wa Ulaya

https://p.dw.com/p/3Fbk9
Theresa May
Picha: Getty Images/J. Taylor

Makubaliano hayo tayari yamekataliwa mara mbili na bunge la Uingereza.

Kulingana na mhariri wa mambo ya siasa wa kituo cha televisheni cha ITV Uingereza, Robert Peston, waziri mkuu Theresa May aliwaambia aliyewahi kuwa waziri wake wa mambo yanje Boris Johnson, Iain Duncan Smith, Steve Baker na wengine wanaounga mkono mpango wa Brexit kwamba angejiuzulu iwapo makubaliano hayo yangepigiwa kura bungeni, na hususan suala la mpaka wa Ireland.

Hata hivyo mhariri huyo alisema, May hakueleza ni wakati gani hasa angeweza kuondoka, kwa hivyo hakukuwa na aliyeamini kama kweli angeondoka.

Haya yanajiri katika wakati ambapo mbunge mmoja wa chama cha Kihafidhina cha May Andrew Bridgen kutamka wazi kwamba waziri mkuu May ambaye amepoteza imani kwa mawaziri wake waandamizi, wabunge pamoja na wajumbe wa chama chake anatakiwa kujiuzulu. Bridgen anaunga mkono Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya bila ya makubaliano.

England, London: Theresa May
Waziri Mkuu Theresa May, anadaiwa kukosa imani na wabunge wake na hata mawaziriPicha: picture-alliance/AP/M. Duffy

Amesema anadhani waziri mkuu May hana imani tena na chama chake. Ameonyesha dhahiri kabisa kwamba hana imani na baraza na hata kwa wanachama wa Conservative walio nje ya bunge. Akahitimisha kuwa angetaka kufanyika kwa chaguzi mpya za kitaifa za kuchagua wabunge wapya ambao wataunga mkono suala la Brexit, lakini hata hivyo, alisema kamwe hataunga mkono juhudi zinazofanywa na chama cha upinzani cha Labour kuiangusha serikali.

Hapo jana, waziri wa nchi anayeshughulikia masuala ya mazingira, chakula na mahusiano vijijini nchini humo Michael Gove aliwaambia waandishi wa habari hilo si chaguo bora kwa wakati huu. 

"Hapana, sidhani kama ni wakati muafaka wa kubadilisha kapteni wa meli. Nadhani tunachotakiwa kufanya ni kukubaliana namna muafaka na waziri mkuu amekwishasema kwamba namna muafaka ni kuhakikisha tunapata makubaliano yatakayoturuhusu kuondoka, huku uchumi wetu ukiendelea kuimarika lakini pia tukiendelea kunufaika  nje ya Umoja wa Ulaya."

UK Brexit l  pro-Brexit leave Demonstration
Waandamanaji wanaounga mkono Brexit. Uingereza bado iko katika sintifahamu kuhusu kuondoka Umoja wa Ulaya.Picha: Getty Images/J. McPhersen

Katika hatua nyingine, chanzo kimoja cha serikali kimearifu kwamba mawaziri wa Uingereza hii leo wanataraji kukutana na kujadiliana kuhusu majaribio ya bunge ya kutaka kuuhodhi mchakato huo wa Brexit kabla baraza hilo halijakutana na waziri mkuu May.

Chanzo hicho kimesema kwa sharti la kutotajwa jina kwamba baraza la May ambalo ni la mawaziri wake waandamizi, baada ya hapo litakutana tena kwa ajili ya majadiliano kuhusu mustakabali wa Brexit, hatua inayotajwa kuwa ni mabadiliko makubwa ya kisera nchini humo.

Aidha, wabunge wa bunge la Uingereza wataangazia hii leo kupiga kura juu ya hatua ya serikali inayofuata kuhusu Brexit, lakini pia nia yake ya kutaka kuuhodhi mchakato huo, huku pia likijaribu kusaka wingi kuhusu njia mbadala ya kusonga mbele ambayo itaondoa mkwamo uliotamalaki ndani ya bunge hilo.   

Uingereza ilitakiwa kuondoka Umoja wa Ulaya ifikapo Machi 29, lakini baada ya kukataliwa mara mbili bungeni kwa mpango wa waziri mkuu May, aliokubaliana na Umoja wa Ulaya kuhusu Brexit, alikubali kuurefusha kwenye mazungumzo kati yake na Umoja huo, Alhamisi iliyopita, hadi Mei 22.

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE

Mhariri:Sekione Kitojo