1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shimon Peres anajitoa kutoka Chama cha labour cha Israel

30 Novemba 2005

Mwanasiasa mkongwe wa Israel, Shimon Peres, leo anatazamiwa kujitoa kutoka chama cha Labour na kukiunga mkono chama cha Kadima cha Ariel Sharon, ambacho, kwa mujibu wa makisio ya uchunguzi wa maoni, kinatazamiwa kuchomoza kuwa mshindi katika uchaguzi mkuu wa mwezi Machi mwakani. Zaidi juu ya uamuzi wa mshindi huyo zawadi ya amani ya Nobel, huyu hapa Othman Miraji…

https://p.dw.com/p/CHLp
Shimon Peres(kushoto) na waziri mkuu wa Israel, Ariel Sharon
Shimon Peres(kushoto) na waziri mkuu wa Israel, Ariel SharonPicha: AP

Baada ya miongo mingi kuwemo katika Chama cha mrengo wa shoto na katikati cha Labour, na akiwa na uzoefu wa zaidi ya nusu karne katika siasa za Israel, mshindi huyo wa tunzo la amani la Nobel anatazamiwa leo kutoa uamuzi wake huo wa kushangaza baada ya kurejea nyumbani kutokea Bacelona.

Katika mahojiano na gazeti linalouzwa kwa wingi nchini Israel, YEDIOT AHARONOT, Shimon Peres yaonesha ameshajiwekea misingi ya kujitoa kutoka chama cha Labour, akisema njia inayopitia taifa ni muhimu zaidi kuliko siasa za vyama. Alisema yeye anajali zaidi juu ya njia ambayo taifa itapitia, na kwake yeye chama cha kisiasa sio muhimu. Alisema cha kujali sio wapi mtu alipo, lakini wapi anakoelekea. Shimon Peres alishikilia kwamba lazima mtu aingoze nchi kuelekea amani, na kwa jambo hilo, alisema, Ariel Sharon, anachukuwa hatua sawa.

Tangazo rasmi juu ya nia hiyo yake litahakikisha zile tetesi zilizoenea tangu mwanasiasa huyo, mwenye umri wa miaka 82, kushindwa katika kinyanganyiro cha uongozi wa chama cha Labour na mkuu wa chama cha wafanya kazi, Amir Peretz, na Ariel Sharon kujitoa kutoka chama cha mrengo wa kulia cha Likud na kuunda chama cha mrengo wa katikati.

Wachunguzi wa mambo wanaamini ushirika wa wanasiasa hao wawili walio wazito ni karata itakayokuwa na nguvu na uzoefu kuweza kuvishinda vibaya katika uchaguzi vyama vya Likud na Labour, hivyo kufanya historia katika suala la mzozo baina ya Wa-Israeli na Wapalastina. Uhariri katika gazeti la YEDIOT ulisema Shimon Peres, ambaye hadi siku chache zilizopita alikuwa anabezwa na duru zilizomzunguka Ariel Sharon, kwa ghafla amegeuka kuwa ni mtu wa faida kwa kundi hilo. Shimon Peres, ambaye mara mbili aliwahi kuwa waziri mkuu, licha ya kwamba hajawahi kushinda uchaguzi, alitupiliwa mbali kutoka serekali ya mseto ya Sharon na akapoteza kiti chake kama naibu wa waziri mkuu baada ya Amir Peretz kukitoa chama cha Labour kutoka serekali ya mseto mwanzoni mwa mwezi huu. Japokuwa ni hakika atamuunga mkono Sharon, lakini haifikiriwi kwamba Shimon Peres atakisaliti kabisa chama cha Labour na kujiunga hasa na Chama cha Kadima. Badala yake huenda akafanywa kuwa mwakilishi maalum wa Ariel Sharon katika masuala ya kutafuta amani au kuteuliwa kuwa mkuu wa juhudi za kuyaendeleza maeneo ya Galillee na Negev ambayo yako nyuma, kimaendeleo.

Tangu Ariel Sharon alipojitoa kutoka Chama cha Likud, akikasirika kutokana na chama hicho kuupinga mpango wake wa kuondosha majeshi ya Israel kutoka Ukanda wa Gaza, uchunguzi wa kura za maoni ya Wa-Israeli unaonesha chama kipya cha Kadima kinavishinda vyama vingine kwa kupendwa na wananchi, hivyo kumpa haki Ariel Sharon katika kamari yake ya kisiasa alioicheza. Uchunguzi unaonesha chama cha Likud ambacho sasa hakina kiongozi na kimezongwa na mabishano makali miongoni wakuu wake kitashindwa vibaya pindi uchaguzi mkuu utafanyika leo. Viti vyake bungeni vitapungua kutoka 40 vya sasa na kubakia 10 katika bunge la wajumbe 120, huku Chama cha Kadima kitapata viti 34, chama cha Labour viti 27 na kile cha Wayahudi wenye siasa za kiasilia, Shas, viti 11. Naye waziri wa mambo ya kigeni wa Israel, Silvan Shalom, mtu anayepigania uongozi wa Chama cha Likud, amedai kwamba Benjamin Netanyahu, mtu anayetegemewa sana kushika usukani wa chama hicho, atakivuruga chama hicho pindi atachaguliwa kuwa kiongozi wake. Alisema Chama cha Likud kiko katika mzozo, na jambo hilo haliwezi kufichwa.

Miraji Othman