Sheria mpya kwa wahamiaji nchini Ujerumani
19 Oktoba 2010Serikali ya kansela Angela Merkel inatayarisha sheria mpya ambayo itawataka wahamiaji kujijumuisha vizuri zaidi katika jamii ya Ujerumani. Msemaji wa serikali amesema mjini Berlin jana kuwa mapendekezo hayo ni pamoja na ulazima wa kusoma lugha ya Kijerumani na mtu anaweza kuadhibiwa ,iwapo atashindwa kumaliza masomo yanayotakiwa kwa ajili ya kujumuishwa. Matokeo kwa mtu atakayeshindwa inaweza kuwa pamoja na kupunguziwa mafao ya kijamii ama kubatilisha ruhsa ya kuishi nchini. Hata hivyo , muswada huo , ambao unatarajiwa kupigiwa kura mwezi Desemba , pia utaimarisha hatua ya kutambua shahada zilizopatikana kutoka mataifa ya kigeni. Kiasi cha wahamiaji wanaokadiriwa kufikia 300,000 wanaoishi nchini Ujerumani kwa hivi sasa wanashindwa kufanyakazi walizojifunza kwasababu masomo waliojifunza hayajathibitishwa na maafisa wa Ujerumani.