1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Shambulizi la Urusi laua mtu mmoja, 23 wamejeruhiwa Mykolaiv

27 Aprili 2023

Mtu mmoja ameuawa na wengine 23 wamejeruhiwa katika shambulizi la anga lililofanywa na Urusi kwenye eneo la makaazi kusini mwa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4QcS9
The building of the "Central Enterprise for the Management of Radioactive Waste" in Chornobyl
Picha: State Agency of Ukraine for Exclusion Zone Management

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema shambulizi hilo limetokea mapema Alhamisi asubuhi katika mji wa Mykolaiv na miongoni mwa waliojeruhiwa ni mtoto mmoja.

Zelensky ameandika katika mtandao wa Telegram kwamba usiku wa kuamkia Alhamisi, Urusi iliushambulia mji wa Mykolaiv kwa makombora manne aina ya Kalibr, ambayo yalirushwa kutoka eneo la Bahari Nyeusi.

Urusi iliyalenga makaazi ya watu

Kwa mujibu wa Zelensky, silaha za kivita ziliyalenga makaazi ya watu binafsi, jengo la kihistoria, na jengo refu lenye ghorofa nyingi. Video iliyochapishwa na Zelensky imeonyesha jinsi majengo hayo yalivyoharibiwa vibaya, huku moshi ukifuka kwenye paa.

Gavana wa Mykolaiv, Vitaliy Kim amesema huduma za dharura zimewekwa. Naye Mkuu wa Kituo cha Pamoja cha Habari kuhusu Kamandi ya Oparesheni, Natalia Humeniuk amesema kuwa juhudi za uokozi zinaendelea, ingawa tayari moto umezimwa.

Ukraine | Krieg | Zerstörung in Cherson
Kifaru cha Ukraine kikiwa katika barabara iliyoko kati ya Mykolaiv and KhersonPicha: Igor Burdyga/DW

Urusi imekanusha kuwalenga kwa makusudi raia katika uvamizi wake nchini Ukraine ambao hadi sasa umesababisha mauaji ya maelfu ya watu, kusababisha mamilioni wengine kuyakimbia makaazi yao na kuharibu miji.

Kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia Haki za Binaadmau, zaidi ya raia 8,000 wameuawa nchini Ukraine, tangu uvamizi huo wa Urusi wa Februari, 2022.

Ukraine kupewa silaha kwa wakati

Huku hayo yakijiri, jenerali wa ngazi ya juu wa Marekani barani Ulaya, ameliambia Bunge la Marekani kwamba jeshi la Ukraine litapatiwa silaha inazohitaji kwa wakati kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi yanayotarajiwa kufanywa na vikosi vya Urusi ndani ya nchi hiyo.

Aidha, mkuu wa kundi la wapiganaji wa kampuni binafsi ya kijeshi ya Urusi ya Wagner, amesema Ukraine inajiandaa kwa mashambulizi ya kujilinda yanayoweza kuepukika na inapeleka vikosi vyake vilivyoandaliwa kwenye mji wa mashariki wa Bakhmut, ulioharibiwa kwa mapigano.

Ama kwa upande mwingine, Zelensky leo amekutana na mshauri wa usalama wa taifa la Uingereza, Timothy Barrow mjini Kiev. Antony David Radakin, afisa wa kikosi cha majini cha Uingereza, pia alihudhuria mkutano huo ambao uliangazia msaada zaidi wa kijeshi kwa Ukraine.

Ukraine Präsident Wolodymyr Selenskyj
Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskyPicha: president.gov.ua

Maafisa wamesema Zelensky ameitolea wito Uingereza kuongoza na kuonesha mfano katika kuunda kile alichokiita ''muungano wa kikosi cha anga'' ili kuisaidia Ukraine kupata ndege za kijeshi.

Wakati huo huo, Waziri wa Kilimo wa Ujerumani, Cem Özdemir amesema Urusi inapaswa kutelekeza ahadi yake ya kuruhusu nafaka kuondoka kwenye bandari za Ukraine, akisema watu wenye njaa kwenye nchi masikini wanahitaji zaidi nafaka hiyo kutoka nje.

Waziri huyo amesema Alhamisi kuwa Rais wa Urusi, Vladmir Putin alikuwa anatumia tena makubaliano ya ngano kama njia ya kutoa shinikizo ili kuendeleza maslahi yake, na kudhoofisha vikwazo vya mataifa ya Magharibi dhidi ya nchi hiyo.

(DPA, AFP, Reuters)